Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS na wadau wakabidhi vyumba 16 vya huduma za dharura za COVID-19 Yambio

Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.
UN Photo/JC McIlwaine
Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.

UNMISS na wadau wakabidhi vyumba 16 vya huduma za dharura za COVID-19 Yambio

Msaada wa Kibinadamu

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kwa kushirikiana na wadau wamekarabati na kukabidhi vyumba 16 vya huduma za dharura kwa ajili ya janga la corona au COVID-19 kwenye kituo cha wagonjwa mahututi mjini Yambio Magharibi mwa jimbo la Equatoria

Mjini Yambio kwenye kituo cha huduma za dharura na wagonjwa mahututi, uongozi wa UNMISS wa eneo hilo ukiambatana na maafisa wa serikali na gavana wa jimbo la Equitoria Magharibi kwenda kufanya makabidhiano ya muhimu ya vyumba 16 vya kituo hicho kwa ajili yakutoa huduma za dharura  za COVID-19. 

Mradi huu umefanywa kwa pamoja na kikosi kazi cha serikali ya Sudan Kusini kinachohusika na COVID-19 ili kuhakikisha kuna kituo maalum kinachojitosheleza kwa ajili ya wagonjwa wa janga hilo. 

Mbali ya kukarabati vyumba UNMISS imekabidhi pia jenereta, vitanda 20 na magodoro yake, mashuka 120 na tangi la maji lenye uwezo wa kujaza lita 5,000. 

Stella Abiyomi ni kaimu mkuu wa ofisi ya UNMISS kwenye jimbo la Equatoria anasema lengo kubwa ni kuisaidia malaka na jamii za Yambio katika maandalizi ya kukabiliana na COVID-19, “yote haya ni kuhakikisha kuna mazingira yanayowezesha kufikisha mahitaji ya kibinadamu kama sehemu ya msaada unaotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa kwa mikakati ya serikali ya kupambana na COVID-19 . UNMISS imeshirikiana na familia nzima ya Umoja wa Mataifa, wadau wa maendeleo na serikali kuhakikisha kwamba tuko tayari kuchukua hatua zinazostahili kwa janga hili linalotupa changamoto sote. Kwa mchango huu kutoka UNMISS tunaamini kwamba kituo hiki cha huduma za muhimu sana kitatumika kwa lengo lililokusudiwa.” 

Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo alikuwa gavana wa jimbo la Equatoria Magharibi Jenerali Alfred Futuyo ambaye ameishukuru UNMISS na kuahidi kukilinda kituo hicho na kuongeza kwamba,“nilianza ukarabati wa hospitali ya kiraia na nataka sote tuchangie, UNMISS, wafanyabiashara na hata mimi ambaye ni gavana nitatoa msaada wangu.” 

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti Sudan Kusini imeripoti wagonjwa wa COVID-19 zaidi ya 2,500 na vifo zaidi ya 47.