Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moratinos achukizwa na kitendo cha Quran Tukufu kuchomwa moto nchini Sweden

Mwakilishi wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa UNAOC Miguel Ángel Moratinos akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka maktaba 2010)
UN Photo/Aliza Eliazarov
Mwakilishi wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa UNAOC Miguel Ángel Moratinos akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka maktaba 2010)

Moratinos achukizwa na kitendo cha Quran Tukufu kuchomwa moto nchini Sweden

Utamaduni na Elimu

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya muungano wa ustaarabu, UNAOC Miguel Moratinos amelaani vikali kitendo cha kuchomwa kwa Quran Tukufu kilichofanywa na watu wenye misimamo mikali kwenye mji wa Malmo nchini Sweden.
 

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake jijini New York, Marekani imemnukuu Bwana Moratinos akisema kuwa kitendo cha ijumaa kilichosababisha maandamano hakikubaliki na hakilalishiki.
“Aina ya vitendo hivi vya kuchukiza vinavyofanywa na walafi wa chuki wakiwemo watu wa mrengo wa kulia uliopitiliza na vikundi vyenye misimamo mikali, vinachochea ghasia na vinamomonyoa jamii zetu,”  amesema Bwana Moratinos .
Amesisitiza kuwa matukio kama hayo ni kinyume na malengo na maadili yanayozingatiwa na ofisi yake ya UNAOC, “ambayo inafanya kazi kuendeleza kuheshimiana na kuelewana na kuimarisha mazungumzo baina ya tamaduni na madhehebu ya dini.”
Mwakilishi huyo amekumbusha kuwa “dharau dhidi ya vitabu vitakatifu na maeneo ya ibada sambamba na alama za kidini inapaswa kuepukwa na waumini wote wa dini.”
Ametoa wito kwa viongozi wa kidini kwenye madhehebu yote kurejelea wito wao wa kukataa aina zote za ghasia kwa misingi ya dini au imani.
Katika muktadha huo, Bwana Moratinos amerejelea azimio namba 73/164 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapiga marufuku ukosefu wa stahmala, fikra hasi, unyanyapaa, ubaguzi, chuki dhidi ya watu kwa misingi ya imani zao au dini zao.