Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

EU yachangia dola milioni 477 kusaka chanjo dhidi ya COVID-19

Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19
UN Photo/Loey Felipe
Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19

EU yachangia dola milioni 477 kusaka chanjo dhidi ya COVID-19

Afya

Kamisheni ya Muungano wa Ulaya, EU leo imethibitisha nia yake ya kushiriki katika mfumo wa COVAX wa kusaka chanjo dhidi ya COVID-19 na itakayopatikana kwa watu wote na popote pale duniani.
 

Taarifa iliyotolewa na kamisheni hiyo leo mjini Brussels, Ubelgiji, imeonesha kuwa pamoja na uthibitisho huo, Kamisheni imetoa mchango wa dola milioni 477 kusaidia malengo ya COVAX katika harakati za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 duniani kote.

Rais wa Kamisheni hiyo, Ursula Von De Leyen amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema kuwa, “ushirikiano wa kimataifa ndio njia pekee ya kutokomeza janga hili. Kupitia hatua za kimataifa za kukabili virusi vya Corona na kampeni ya lengo la kuunganisha dunia dhidi ya vita hivi, tumeona ulimwengu ukiwa kitu kimoja.”

Ameongeza kuwa,  “zaidi ya dola bilioni 19 zimeshapatikana kama ahadi hadi hivi sasa na watafiti wenye vipaji na mashirika wanaunganisha nguvu zao kupata chanjo, vitendanishi na tiba, ambavyo vitatumika duniani kote, kwa maslahi ya wote. Leo kamisheni inatoa dola milioni 477 kuchangia COVAX kwa lengo la kushirikiana kununua chanjo za baadaye kunufaisha nchi za kipato cha chini na kati. Nina imani hii inatusogeza karibu kwenye lengo letu, kutokomeza virusi pamoja.”

Mfumo wa COVAX ukisimamiwa pamoja na ubia wa chanjo duniani, GAVI na ushirika wa maandalizi dhidi ya milipuko, CEPI na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, unalenga kuchagiza utengenezaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 na kuhakikisha kuwa kila mtu popote pale alipo duniani anaipata bila kikwazo chochote.