Ubia wa UNICEF na serikali Uganda waleta nuru kwa waishio na VVU 

31 Agosti 2020

Nchini Uganda, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, kwa kushirikiana na serikali, limechukua hatua kuhakikisha kuwa huduma za msingi za kiafya za kuokoa maisha ikiwemo dawa za kupunguza makali ya UKIMWI zinapatikana hata wakati huu wa vizuizi vya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. 

Katika wilaya ya Yumbe, iliyoko maeneo ya mpakani nchini Uganda, vizuizi vitokanavyo na ugonjwa wa Corona au COVID-19 vimekuwa ni changamoto kubwa kwa wakazi wengi. 

Wananchi wamekabiliwa na changamoto kufikia huduma za afya na wale walio hatarini, mathalani waliokuwa wanahitaji dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI, wamekuwa hatarini zaidi. 

Rabind Dare ambaye ni mtaalamu wa afya wa UNICEF anasema imekuwa vigumu kwa watoa huduma na wahudumiwa kupata huduma za afya.  

UNICEF na serikali ya Uganda walibaini pengo hilo na kuchukua hatua kama asemavyo Dkt Raphael Yayi, Afisa wa afya wilaya ya Yumbe, “vizuizi vilipoanza na tukaona kuwa ufikiaji huduma ni tatizo na tukaanza kupoteza wateja  hasa wale wanaoishi na VVU ambao walitakiwa kuchukua dawa zao, walikuwa hawafiki tena. Halikadhalika tuliona huduma zetu kwenye vituo vya afya zilianza kuporomoka. Kwa msaada wa fedha kutoka UNICEF tulijipanga upya kushughulikia changamoto hizo.” 

Kilichofanyika ni kutumia mifumo iliyokuwepo ambapo wataalamu wa afya wa vijiji walitembelea majumbani watu wanaoishi na VVU na wanapatiwa dawa zao kwa usalama na kwa faragha kama asemavyo Beatrice Baru mtaalamu wa VVU, "namuuliza ridhaa yake iwapo anaweza kupokea dawa akiwa nje au ndani, kisha tunaingia chumbani, nampatia ushauri nasaha na kumuuliza anajisikiaje anapokunywa dawa, akisema yuko sawa, basi namwambia nimempatia dawa za miezi mitatu na akishaweka saini, basi nampatia dawa.” 

Pamoja na wataalamu wa VVU, UNICEF Uganda imeanzisha bodaboda za kubeba wajawazito wanakaribia kujifungua, ambapo mama akiwa kwenye uchungu, dereva wa bodaboda anapatiwa taarifa na kumpeleka hospitali ya juu zaidi. 

Hivi sasa UNICEF Uganda inasema kuwa idadi ya wanaosaka huduma imeongezeka ikiwemo zile za wajawazito na watoto, sambamba na kufuatilia wanaoishi na VVU. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter