Utoweshwaji binadamu umekithiri duniani, tuchukue hatua – Guterres

30 Agosti 2020

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kukumbuka manusura na waathirika wa kitendo cha kutoweshwa duniani, Umoja wa Mataifa unataka mataifa yote kuazimia upya kuondokana na uhalifu huu wa watu kupotezwa.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wito wake huo unazingatia ukweli kwamba uhalifu huo umeenea kote duniani na kila uchao kuna ripoti za watu kutoweka wakiwemo watetezi wa mazingira ambao amesema mara nyingi ni watu wa jamii ya asili.

"Wakati huo huo machungu ya wale waliopotea bado yapo na maelfu yao hata hawajulikani waliko, na hivyo kufanya uhalifu huu kuendelea kusababisha majonzi kwa familia za waliotoweshwa," amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa Kamati ya Umoja wa Mataifa na kikundi kazi kuhusu watu waliotoweshwa kimebaini mienendo ya kutia wasiwasi, ikiwemo visasi dhidi ya jamaa za waliotoweshwa au wafuasi wa vikundi vya kiraia na mara nyingi visingizio vya kuwafuatilia huwa ni usalama au harakati za kukabili ugaidi.

@UN
Kundi la wataalam wa haki za binadamu kuhusu kutoweshwa au kutoweka pasi hiyari

"Kutoweshwa pia kuna athari za kijinsia na kuathiri zaidi wanawake na wale waliobadili jinsia na mashoga," amesema Katibu Mkuu Guterres.

Ameongeza kuwa ukwepaji sheria kwa watekelezaji wa vitendo hivyo kunaongeza machungu zaidi akisema kuwa, "chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, familia na jamii zina haki ya kutambua ukweli kuhusu kilichotokea. Natoa wito kwa nchi wanachama kutekeleza wajibu huu."

Guterres amesema kwa msaada wa mifumo ya kimataifa ya haki za binadmau, nchi zina wajibu wa kuimarisha juhudi zao kuepusha utoweshwaji raia wao, kusaka waliopotea na kuongeza msaada kwa manusura na waathirika wa vitendo hivyo pamoja na familia zao.

"Ni muhimu vile vile kufanya uchunguzi wa kina usio na upendeleo wowote," amesema Katibu Mkuu akitamatisha kwa kutaka kila nchi irejelee azma yake ya kuondokana na utoweshwaji wa watu.

Ametoa wito pia kwa nchi kuridhia mkataba wa kimataifa wa kulinda watu wote dhidi ya kutoweshwa na kukubali uwezo wa Kamati ya kuchunguza madai ya watu.

Guterres amesema hiyo ni hatua ya kwanza, lakini muhimu katika kuondokana na uhalifu huu wa kikatili.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud