Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Natiwa moyo na angalau kuwepo kwa misimamo ya pamoja baina ya pande kinzani Syria- Pedersen 

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataif kwa Syria, Geir O.pedersen akizungumza na wanahabari. (PIcha ya maktaba)
UN Photo/Evan Schneider
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataif kwa Syria, Geir O.pedersen akizungumza na wanahabari. (PIcha ya maktaba)

Natiwa moyo na angalau kuwepo kwa misimamo ya pamoja baina ya pande kinzani Syria- Pedersen 

Amani na Usalama

Wajumbe wa pande kinzani nchini Syria wanaokutana mjini Geneva, Uswisi kwa lengo la kusaka suluhu ya kudumu na kumaliza mzozo wa takribani muongo mmoja nchini mwao, angalau wamekuwa na misimamo inayofanana itakayoweza kusongesha mbele majadiliano, amesema Geir Pedersen, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo wa Syria.
 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, baada ya mazungumzo na pande hizo kinzani yaliyoanza siku ya Alhamisi, Bwana Pedersen amesema, “baada ya wiki yenye changamoto katika mazungumzo ikiwemo kuanza na kukoma, na pia baadhi ya wajumbe kupimwa na kubainika kuwa na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 siku ya Jumatatu, hatimaye wajumbe waliweza kupata baadhi ya maeneo ambayo misimamo yao inafanana.”

Hata hivyo amesema bado kuna kutokukubaliana katika maeneo kadhaa na “unafahamu marafiki zangu hawa wa Syria katu hawachelei kuelezea kile wasichokubali. Lakini pia unafahamu, nimefurahishwa sana kusikia wenyeviti wenza wawili wakisema bayana kuwa wanafikiria kuwa kulikuwepo na maeneo ambayo misimamo yao inafanana. Na kile ambacho nasubiri kwa hamu ni lini tunakutana tena, na tutaweza kuendeleza kutokana na misimamo hiyoya pamoja na kusongesha mbele mchakato wetu.”

Bwana Perdesen ameongeza kuwa, “nina imani kuwa tutaweza kujenga imani kiasi, na kuamiinana na tunaweza kuendelea na kazi yetu ambayo tumeianza, tutaona maendeleo kwenye kazi ya kamati. Lakini kama nilivyosema, maendeleo yapo na kwa kweli ni jukumu la wasyria wenyewe waliomo ndani ya kamati.”

Watoto wakiwa nje ya hema katika kambi ya watu waliotawanywa huko Idlib, kaskazini mwa Syria.
UNOCHA
Watoto wakiwa nje ya hema katika kambi ya watu waliotawanywa huko Idlib, kaskazini mwa Syria.

Matumaini ya kuwepo kwa viashiria vya kuamiana kutoka serikali ya Syria na upinzani ikiwemo hatua za kuachia huru mateka na wafungwa, ni jambo ambalo limekuwa linayoyoma, kwa mujibu wa mjumbe huyo maalum wa UN kwa Syria ambapo ameongeza, “suala la mateka, wafungwa na watu waliotoweshwa kama mjuavyo, yamekuwa ni moja ya vipaumbele vyangu vitano tangu nianze jukumu hili, na ni eneo ambalo nina hofu kuwa hatujaona maendeleo yoyote. Lakini bila shaka, ni matumaini yangu kuwa kutokana na utulivu unaoendelea nchini Syria na kisiasa, tunaweza pia kuona mabadiliko kwenye masuala hayo.”

Akigusia kwa umakini mchakato huo wa Geneva kuhusu amani nchini Syria, kwa kuzingatia uwepo wa mashirika ya kikanda na ya kimataifa nchini Syria, Bwana Pedersen ametoa wito kwa sitisho la mapigano nchini kote, kando mwa makubaliano tete ya kusitisha mapigano ambayo yanazingatiwa kaskazini-magharibi mwa Syria.

Kikao hiki cha tatu cha kamati ya kikatiba kuhusu Syria kinachoratibiwa na Umoja wa Mataifa kimefanyika baada ya mapumziko ya miezi 9 yaliyosababishwa na tofauti kuhusu ajenda ambazo hatimaye zilipatiwa suluhu mwezi Machi na kisha kufuatiwa na vikwazo vilivyotokana na COVID-19.

Majadiliano ya awali kuhusu mundo wa kamati hiyo yalifanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana wa 2019 mjini Geneva.

Kamati hiyo ina wajumbe 150, ambapo 50 waawakilishi serikali ya Syria, 50 upande wa upinzani na 50 wanatoka mashirika ya kiraia nchini Syria wakiwakilisha madhehebu ya dini, makabila na maeneo tofauti ya kijiografia.