Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pamoja na vikwazo vya COVID-19, UNICEF yaendelea kupambana na utapiamlo DRC 

Picha kutoka maktaba ikimewonesha mhudumu wa afya akimtibu mmoja ya watoto waathirika wa utapiamlo Kasai DRC (2017)
Picha ya UNICEF/UN064905/
Picha kutoka maktaba ikimewonesha mhudumu wa afya akimtibu mmoja ya watoto waathirika wa utapiamlo Kasai DRC (2017)

Pamoja na vikwazo vya COVID-19, UNICEF yaendelea kupambana na utapiamlo DRC 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limeendelea na juhudi zake za kusaidia kupambana na utapiamlo kwa watoto nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ingawa COVID-19 inatishia shughuli hizo znazolenga kuwaokoa watoto wapatao milioni 3.4. 

Ingawa utapiamlo nchini DRC unashuhudiwa zaidi katika maeneo yenye vita kama vile mashariki mwa nchi hiyo, lakini juhudi za kutibu na kupambana na utapiamlo mkali unaotishia maisha ya watoto zinahitajika kote nchini humo. 

Hapa ni katika eneo la Nsele, moja ya viunga vya mji mkuu wa DRC, Kinshasa kwa ufadhili wa UNICEF, akina mama na walezi wakiwa  wamewaleta watoto wao ili wapimwe uzito, kupewa dawa na pia kuelimishwa kuhusu mlo bora.  

Watoto wanapimwa uzito mmoja baada ya mwingine kisha kwa kutumia kipimo cha kupima mzingo wa mkono wataalamu wanaweza kutambua mtoto ameathirika kwa kiasi gani na utapiamlo. Kipimo kikizunguka mkono hadi katika rangi nyekundu, ni dhahiri afya ya mtoto iko mashakani n ani wazi amekosa mlo wa bora wa kutosa.  

Mama huyu mwenye umri wa miaka 19 ni miongoni mwa waliofika hapa na anasubiri zamu yake kumpima binti yake Juliana mwenye umri wa miezi 11. Hapa pia muhudumu wa afya anamminia mdomoni mtoto kidonge cha maji chenye vitamin A.  

Mhamasishaji wa jamii anatoa maelezo kwa akina mama kuhusu upishi, nao wamekaa wakifuatilia kwa makini. Merveille bado yuko hapa akiwa amempakata mtoto wake anafuatilia jinsi ya kuandaa na chakula na anaeleza kwa nini anaona ni muhimu kufuatilia tukio zima, “Jina langu ni Merveille. Tunakutana hapa kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi. Tangu nilipokuwa mjamzito, nimekuwa nikija hapa kwenye nyumba ya Mama Kevani ambapo tunakutana na tunajifunza jinsi ya kulea watoto wetu. Tunapokuja hapa, wanatufundisha jinsi ya kuwalisha watoto watoto wetu. Nilipompata mtoto wangu niliendelea kuja kwa mama Kevani kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi. Ananifundisha jinsi ya kumtunza mtoto wangu. Nilipojifungua nilimyonyesha mtoto wangu kwa miezi sita, nikaanza kumpa vyakula vyenye virutubisho na sasa ana umi wa miezi 11. Hapa pia tunafundishwa jinsi ya kujikinga. Tunanawa mikono yetu mara kwa mara, tunavaa barakoa, umbali wa mita moja, hatuzururi pasina sababu. Ugonjwa unatutisha, kwa kuwa umesambaa dunia nzima.”