Watu zaidi ya 360,000 wametawanywa na machafuko Chad:IOM 

28 Agosti 2020

Watu wanaokadiriwa kuwa 363,807 hivi sasa wametawanywa katika jimbo la ziwa Chad la Lac linalopakana na Cameroon, Nigeria na Niger limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM. 

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, idadi hiyo ni zaidi ya nusu ya watu wote wa jimbo la Lac na nyenzo ya IOM ya kufuatilia takwimu za watu waliotawanywa kutokana na shughuli za kibinadamu DTM , imebaini kwamba kutokuwepo utulivu kutokana na shughuli za waasi kwa muda mrefu, mabadiliko ya tabianchi na mazingira mabaya ndio sababu kuu za watu kutawanywa hivi karibuni. 

Takwimu gizi zinaashiria ongezeko la asilimia 22 ya idadi ya watu waliotawanywa ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi Aprili mwaka huu wa 2020 na hii ni idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa tangu IOM ilipoanza utekelezaji wa DTM. 

Wakati janga la corona au COVID-19 nalo likizua zahma IOM inasema jimbo lilo la ziwa Chad linakabiliwa na migogoro miwili mikubwa, wa usalama na wa kimazingira. 

Tangu mwaka 2015 jimbo hilo limekuwa mlengwa wa mashambulizi ya mara kwa matra kutoka kwa makundi yenye silaha yanayoendesha uasi kwenye bonde la Ziwa Chad ambalo linajumuisha nchi za Cameroon, Chad, Niger na Nigeria, uasi ambao umewalazimisha mamilioni ya watu kufungasha virago katika nchi hizo nne na kuzikimbia nyumba zao. 

Mkuu wa IOM katika ofisi ndongo ya Bagasola kwenye jimbo la Lac  Mouftah Mohamed amesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu ,mashambulizi na uvamizi unaofanywa na makundi ya watu wenye silaha yamekuwa yakijirudia na kuifanya serikali ya Chad kutangaza mwezi Machi mwaka huu kwamba majimbo mawili yaliyoko kwenye ziwa Chad ya Fouli na Kaya kuwa ni uwanya wa vita. 

"Mwaka huu jimbo hilo la Ziwa Chad limekabiliwa na mvuakubwa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 30. Kwa mujibu wa kipimo cha uhakika wa chakula , tuna mvua inayonyesha ya mm400 na bado inaendelea. Ndio maana tunashuhudia mafuriko makubwa katika vijiji na mashambani ambayo yamewaacha maelfu ya watu wakitawanywa. Mwenendo huu unatia hofu kwani sio tu unajirudiarudia akini idadi ni kubwa na inaendelea kutokana na matatizo ya usalama na hali ya kimazingira’ amesema Anne KathrinSchaefer mkuu wa IOM nchini Chad. 

Na kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba “Ni muhimu sana kuchukua hatua zaidi za kuingilia suala hili na kuimarisha mnepo kwa jamii na ukanda mzima na kusaidia wat una jamii zao kujikwamua haraka iwezekanavyo kutoka kwenye hali hii.” 

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud