Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo tuliyoyapata yatatufikisha kwenye lengo namba 5 la SDGs-Wasichana Tanzania

Wasichana wakisikiliza kwa makini mafunzo ya upigaji picha yaliyoandaliwa na Imani Nsamila jijini Dar es salaam Tanzania.
UN/Imani Nsamila
Wasichana wakisikiliza kwa makini mafunzo ya upigaji picha yaliyoandaliwa na Imani Nsamila jijini Dar es salaam Tanzania.

Mafunzo tuliyoyapata yatatufikisha kwenye lengo namba 5 la SDGs-Wasichana Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wasichana 28 nchini Tanzania wamenufaika na mafunzo ya upigaji picha yalifanywa na mpiga picha maarufu nchini humo, Imani Nsamila, kwa kushirikiana na shirika la Ladies Joint Forum na Kikoi innovative media. Ni mafunzo yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia katika tasnia hiyo inayozidi kukua katika zama hizi za ukuaji wa teknolojia ya dijitali.

Rona Emmanuel Katuma ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi anasema mafunzo haya si tu yatamsaidia katika masomo yake ya sayansi ya uchumi wa majengo, lakini pia kwake hii ni fursa ya kujiajiri. 

Mafunzo haya yatanisaidia mimi kwa namna tofauti kwasababu kama tunapoambiwa kwamba sasa hivi kujiajiri ndio mpango mzima hamna ajira mtaani kwa hiyo kwa sababu hiyo mafunzo haya yatanisaidia kuweza kujiajiri katika namna tofauti na kwa sababu napenda pia kufanya documentary za safari na Mazingira na mambo mbalimbali katika jamii mafunzo haya yatanisaidia sana sana katika kazi hiyo.

Mwingine aliyenufaika na mafunzo haya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ni msichana mdogo Anna Mary Erasto ambaye amehitimu masomo yake ya kidato cha sita. Yeye anasema katika uandishi wake wa makala alikuwa analazimika kutumia picha za wengine, lakini sasa amegundua anaweza kutumia picha zake. 

Kuna wavuti Imani Nsamila anataka kuanzisha ambayo inashughulika na mambo ya picha tumeona kwamba ata sisi kumbe tunaweza kufanya kitu cha namna hiyo kwamba unatengeneza wavuti ambapo unaweka picha zako zote alafu badala ya kutoa picha kwa mtu mwingine wewe mwenyewe ukawa unafanya hicho kitu kwa kutumia zile picha unaweza ukauza kwa watu kwani wanapozitoa kwenye mtandao nawe pia unapata kipato chako. Lakini hata wewe mwenyewe kwa vile itakuwa katika kuandika zile hadithi zile picha utakazokuwa kumeweka kwenye wavuti unaweza kuzitumia katika ile hadithi na kumbuka wewe pekee utakaye kuwa unatumia zile picha kwani kuna watu wengine ambao pia watakuwa wanaandika hadithi tofauti na kutumia zile picha

Salha Ally yeye anasema alichokipata katika mafunzo ya upigaji picha ni kikubwa zaidi kuliko hata alivyofikiri awali,  

Nilikuwa na mawazo madogo lakini nikaenda kujaziliwa zaidi ,nilikuwa tu najua tunafundishwa kuhusu camera, mpiga picha ni nani lakini ndani ya mafunzo ilikuwa ni zaidi ya hayo .Kwa hivyo nikajifunza kwamba kama sasa hivi tunavyokwenda katika masuala ya usawa wa jinsi lengo la tano la malengo ya  maendeleo endelevu naona kabisa kwamba programu hii inawainua kabisa wanawake wapigaji picha kwa maana kwamba sasa tutalingana sawa na wanaume ingawa sasa wanaume ni wengi lakini programu inatulenga sisi wanawake kwa hivyo tunaweza kusoma na kuweka maanani  malengo 17 ya maendeleo endelevu  hasa lengo nambari tano,nilipenda.