Mamilioni ya wakimbizi Afrika Mashariki wako njia panda baada ya mgao wa chakula kukatwa:WFP

Mwanamke akipokea msaada wa chakula kutoka kwa WFP
WFP/Rafael Campos
Mwanamke akipokea msaada wa chakula kutoka kwa WFP

Mamilioni ya wakimbizi Afrika Mashariki wako njia panda baada ya mgao wa chakula kukatwa:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Njaa kubwa na utapiamlo vinawanyemelea mamilioni ya wakimbizi Afrika Mashariki baada ya mgao wa chakula wanaoutegemea kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP kupunguzwa zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Nairobi Kenya changamoto za janga la corona au COVID-19 zimesababisha ufadhili muhimu kutoka kwa wahisani kupunguzwa. 

Tayari shirika hilo lilikuwa limeshalazimika kupunguza mgao wa chakula au fedha hadi asilimia 30 kwa wakimbizi zaidi ya milioni 2.7 nchini Ethiopia, Uganda, Kenya, Sudan Kusini na Djibouti. 

Na sasa WFP italazimika kupunguza zaidi mgao inaotoa katika miezi ijayo endapo haitapokea kwa wakati fedha zaidi kutoka kwa wahisani.  

Akizungumzia changamoto hiyo mkurugenzi wa WFP wa kanda ya Afrika Mashariki Michael Dunford amesema “wakimbizi wako katika hatari kubwa ya kusambaa kwa janga la COVID-19 kwa sababu wanaishi katika mrundikano mkubwa makambini ambako pia hakuna huduma za kutosha za malazi, afya na fursa ya maji safi na usafi” .

Ameongeza kuwa wakimbizi wanakabiliwa na vyote gonjwa la COVID-19 na athari za kiuchumi na kijamii za janga hilo, huku wwanawake , watoto na wazee wakitaabika zaidi na kuwa katika hatihati ya kupata utapiamlo utakaowaongezea zahma.  

Dunford ameongeza kuwa “Wakati kilele cha ugonjwa huo bado hakijafikiwa Afrika Mashariki hatuwezi kuwatelekeza watu ambao wamelazimika kukimbia na kukwama mkambini. Wengi wameshapoteza fursa za kujipatia kipato kutokana na vikwazo vya COVID-19." 

  Hivi sasa WFP inahitaji dola milioni 323 ili kusaidia mamilioni ya wakimbizi ukanda huo wa Afrika Mashariki kwa miezi 6 ijayo, ombi likiwa ni asilimia 22 zaidi ya ilivyokuwa wakati kama huu mwaka jana.