Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la ACAKORO lawa mkombozi wa elimu kwa watoto masikini wa Korogocho Kenya:UNICEF

Mvulana mwenye umri wa miaka 10 akisaidiwa na mama yake mzazi kusoma nyumbani kwenye makazi duni ya Mathare katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
© UNICEF/Translieu/Nyaberi
Mvulana mwenye umri wa miaka 10 akisaidiwa na mama yake mzazi kusoma nyumbani kwenye makazi duni ya Mathare katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Shirika la ACAKORO lawa mkombozi wa elimu kwa watoto masikini wa Korogocho Kenya:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la kijamii la ACAKORO limekuwa mkombozi mkubwa wa elimu kwa watoto masikini wa mtaa wa mabanda wa Korogocho nchini Kenya baada ya shule kuendelea kufungwa kutokana na janga la corona au COVID-19 hadi Januari 2021. ACAKORO linapata ufadhili kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na linatumia njia zote ikiwemo mitandao na hata simu za mkononi kuhakikisha watoto hao masikini wanaendelea na elimu.

Huyo ni Diana Anyango mkazi wa mtaa wa mabanda wa Korogocho na mmoja kati ya maelfu kwa maelfu ya wanafunzi nchini Kenya ambao sasa wanalazimika kusomea nyumbani kutokana na janga la COVID-19 jambo ambalo si rahisi “Tangu wakati corona ilianza, sasa tunasomea tu nyumbani. Mama anaongea na mwalimu kwa Whatsapp, mwalimu anatutumia masomo na wakati mwingine hata vitabu na hata mazoezi tunafanya mama anasahihisha” 

Na changamoto sio kwa wanafunzi tu hata wazazi. Beatrice Akinyi ni mama wa Diana “Wakati watoto walipofunga shule nilipata changamoto sikujua nitafanya nini” 

Na kwa wazazi wengine kama Beatrice Khaliya mtihani ni mkubwa zaidi “Mimi siwezi kumudu simu ya kisasa inabidi niombe kwa jirani, ananiazima ndio niweze kujua leo watoto wanafanya somo gani au ni somo gani limetumwa. 

Na hapo ndipo shirika la kijamii la ACAKORO likachukua nafasi kwa ufadhili wa UNICEF linahakikisha watoto hawa wanaendelea na masomo na wasioweza kumudu kupata masomo mtandaoni wanawafikishia hadi nyumbani. Afisa mkuu wa operesheni wa ACACKORO ni Mohammed Rashid “Kama taasisi ambayo inathamini elimu ACAKORO imekuwa ikitoafursa za kusoma majumbani kwa watoto wetu” 

Hali inayowapa watoto kama Diana matumaini ya kutimiza ndoto zao "Mie nasoma nikiwa mkubwa nataka kuwa mwandishi wa Habari” 

UNICEF mbali ya kufadhili mashirika kama ACAKORO inaisaidia serikali ya Kenya kuhakikisha hakuna mtoto atakayesalia nyuma kielimu kama anavyosema Constance N’dri Kouakou Kouadio mtaalam wa elimu wa UNICEF nchini Kenya “Wakati shule zinatarajiwa kufunguliwa mwezi Januari 2021, UNICEF inatoa msaada kwa serikali ya Kenya ili kuongeza fursa ya watoto kusomea majumbani na kuziandaa vyema shule kwa ajili ya kufunguliwa.” 

Ameongeza kuwa UNICEF inaona itakuwa ni kwa faida ya watoto kurejea shuleni kwani kukaa nyumbani kwa muda mrefu kuna madhara mengi ikiwemo kuzidisha ukatili kwa watoto.