Uwezekano wa kuambukizwa COVID-19 kwa mara ya pili ni mdogo- WHO

25 Agosti 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema kuna uwezekano mdogo sana kwa mtu kuambukizwa zaidi ya mara moja ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. 

Msemaji wa WHO Dkt. Margaret Harris akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema kauli yao inafuatia ripoti kutoka Hong Kong kuhusu mwanaume ambaye ameambukizwa virusi vya Corona kwa mara ya pili baada ya kupona zaidi ya miezi minne iliyopita. 

Dkt. Harris ameondoa watu wasiwasi ya kwamba taarifa hizo zinaweza kuleta hofu mpya na kwamba“muhimu au jambo jingine muhimu la kutambua ni kwamba idadi ya watu wanaoambukizwa kwa mara ya pili ni ndogo mno. Hiki ni kisa kimoja kilichoripotiwa miongoni mwa zaidi ya watu milioni 23 walioambukizwa COVID-19 duniani kote na tunaweza kuona mgonjwa mwingine. Lakini inaonekana si kitu cha mara kwa mara kinachojirudia, tungalikuwa tumeshapata idadi kubwa.” 

Hata hivyo Dkt. Harris amesema kuwa taarifa hizo za mgonjwa kuambukizwa mara ya pili si za kupuuzia na kwamba kwa mujibu wa wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Hong Kong, aina ya virusi ambavyo aliambukizwa mwanaume huyo miezi minne baada ya kuugua COVID-19 kwa mara ya kwanza walikuwa ni tofauti. 

Jambo muhimu hapa hizi ni taarifa muhimu. Tumeshakuwa na ripoti kila wakati za mtu kuonekana hana virusi na kisha anapimwa tena anakutwa na virusi. Na hadi sasa haijawa dhahiri kuwa iwapo kulikuwa na tatizo katika uchukuaji wa vipimo au watu waliambukizwa mara ya pili,” amesema Dkt. Harris. 

Amesisitiza kuwa vipaumbele vya WHO hivi sasa ni kuelewa maana yak inga ya mtu mwilini “na ndio maana hivi sasa tuna tafiti nyingi zinafuatilia watu kupima vikinga mwili vyao na vile vile kutambua kinga ya asili ya mtu mwilini inadumu kwa muda gani na hilo linapaswa kueleweka kwa kuwa ni tofauti na kinga ambayo mtu anapata kutokana na chanjo.” 

Hadi leo Agosti 25, watu takribani milioni 23.5 wameambukizwa COVID-19 duniani kote na kati yao hao zaidi ya 809,000 wamefariki dunia. 

Eneo lililoathirika zaidi na COVID-19 ni Amerika likiwa na wagonjwa zaidi ya milioni 12.5, likifuatiwa na Ulaya wagonjwa milioni 3.995, Asia kusini-mashariki wagonjwa milioni 3.666, Mediteranea mashariki wagonjwa milioni 1.8, Afrika ikiwa na wagonjwa milioni 1 ilhali ukanda wa Pasifiki Magharibi una wagonjwa 460,991. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter