Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaelekeza meli yake yenye shehena za vyakula Lebanon ili kunusuru wananchi

 Usafirishaji wa tani 12,500 za unga wa ngano uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP unapakuliwa katika Bandari ya Beirut, Lebanon.
WFP/Malak Jaafar
Usafirishaji wa tani 12,500 za unga wa ngano uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP unapakuliwa katika Bandari ya Beirut, Lebanon.

WFP yaelekeza meli yake yenye shehena za vyakula Lebanon ili kunusuru wananchi

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limefikisha tani 12,500 za unga wa ngano nchini Lebanon ili kuepusha ongezeko la bei ya mkate nchini humo kwa mwezi wote wa Septemba unaoweza kusababishwa na milipuko mikubwa ya tarehe 4 mwezi huu wa Agosti iliyosambaratisha bandari ya Beirut ambayo ni tegemeo kwa kupokea shehena za mizigo katika taifa hilo la Mashariki ya Kati. 

Tayari Wizara ya Uchumi na Biashara nchini humo na wasagishaji nafaka na waoka mikate wamefikia makubaliano ya mgao wa shehena hiyo kupitia mifumo iliyopo ili kuepusha rabsha kwenye soko. 

Lebanon huagiza kutoka nje takribani asilimia 85 ya chakula chake na kiwango kikubwa hupitia bandari ya Beirut ambayo kuharibiwa kwake na milipuko kunaweza kusababisha ongezeko la bei za vakula ambazo tayari zilishaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa mwaka mmoja uliopita. 

Mkurugenzi wa Operesheni za WFP nchini Lebanon, Amer Daoudi akizungumzia hali ya bandari ya Beirut amesema kuwa, “maeneo yote ya kuhifadhi nafaka yameharibiwa. Vinu vyote vya kuhifadhia nafaka vimeharibiwa. Hapa ni eneo pekee katika Lebanon nzima ambalo lina uwezo wa kupokea shehena kubwa na nyingi ya nafaka, iwe ni kwa ajili ya kutengeneza mikate au chakula cha mifugo. Eneo la kuhifadhi limeharibiwa kabisa. Mifumo yote ya kupakua na kupakia imesambaratishwa.” 

Ili kusaidia wananchi wa Lebanon, WFP imefikisha meli yake yenye shehena ya ngao kwenye bandari ya Beirut ambako wafanyakazi wake wanajenga bohari ya muda huku Bwana Daoudi akisema kuwa, “tuko katika mchakato wa kuleta vifaa vya kuongeza uwezo na kurejesha uwezo wa bandari ya Beirut ili iweze kupokea mizigo mingi.” 

Wakazi wa Karantina nao wahaha, familia zashindwa kujikimu 

Kwa wakazi wa eneo la Karantina lililo jirani na bandari ya Beirut, milipuko iliharibu kwa kiasi kikubwa makazi yao. 

Miongoni mwa wakazi hao ni Omar Hussein ambaye ni kibarua na siku ya mlipuko, alijikuta amerushwa hadi ardhini na kufunikwa na vifusi vya vioo vilivyovunjika. 

Hivi sasa yeye na familia yake wanahaha kupata usaidizi akisema kuwa, “hata kabla ya milipuko, hali ilikuwa mbayá sana. Mimi na mke wangu tunahitaji dawa zinazogharimu dola 560 na hatuna msaada zaidi ya Mungu. Watoto wetu walikuwa wanatusaidia hadi dola 46, lakini baada ya maandamano na kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, hawana tena ajira. Hii imetufanya tusalie takribani miezi 2 bila dawa.” 

Janga la mlipuko Beirut limekuja wakati Lebanon inakabiliwa na janga kubwa la kifedha kuwahi kukumba nchi hiyo, ukosefu wa ajira ukiongezeka, familia zikihaha kunusuru maisha yao. 

Hivi sasa zaidi ya wananchi milioni 1 nchini Lebanon ni maskini wa kupindukia huku Benki ya Dunia ikikadiria kuwa watu 841,000 ni hohehahe. 

WFP imepanga iwapo itapata fedha itapanua programu yake ya msaada wa kifedha ili iwafikie watu wengi zaidi nchini Lebanon, wakiwemo waathirika wa milipuko ya Beirut na wale wanaohaha kutokana na janga la kiuchumi na hatua za kutochangamana zitokanazo na COVID-19. 

Shirika hilo linakadiria kuwa ili kukidhi msaada wake wa dharura Lebanon, linahitaji dola milioni 235 kwa miezi 6 ijayo ili liweze kusambaza chakula kwa walio na uhitaji zaidi.