Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID 19 imeathiri utalii na hivyo kuharibu ajira, uchumi na urithi wa asili-Guterres

Watalii nchini India wakitumia usafiri wa tembo kupanda katika eneo la mnara wa Amber nje kidogo ya Jaipur.
Eric Ganz
Watalii nchini India wakitumia usafiri wa tembo kupanda katika eneo la mnara wa Amber nje kidogo ya Jaipur.

COVID 19 imeathiri utalii na hivyo kuharibu ajira, uchumi na urithi wa asili-Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia tamko lake la kisera kuhusu utalii na COVID-19, amesema imeleta maumivu makali kuona jinsi ambavyo utalii umeharibiwa na janga la COVID-19. 

Bwana Guterres akizungumza kwa njia ya video amesema utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zaidi ulimwenguni na sekta hiyo natoa ajira kwa mtu mmoja katika kila watu kumi duniani huku ikitoa riziki kwa mamilioni zaidi ya watu. 

“Inakuza uchumi na kuwezesha nchi kustawi. Inaruhusu watu kuendeleza utajiri wa kitamaduni na asili na kuwaunganisha watu na kuonyesha utu wetu. Kwa kweli, mtu anaweza kusema kuwa utalii wenyewe ni moja ya maajabu ya ulimwengu. Ndio maana imeleta maumivu makali kuona jinsi ambavyo utalii umeharibiwa na janga la COVID-19.” Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya
World Bank/Curt Carnemark
Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya

Ajira zimeathirika  

Bwana Guterres akieleza tathimini ya athari ya COVID-19 kwa utalii ameeleza kuwa katika miezi mitano ya mwanzo wa mwaka huu wa 2020, zaidi ya nusu ya watalii wanaowasili kimataifa walipungua na hivyo dola bilioni 320 katika mauzo ya nje kutokana na utalii zilipotea. 

Aidha Bwana Guterres ameeleza kuwa kwa jumla, ajira za moja kwa moja milioni 120 katika utalii ziko hatarini. Wengi wako kwenye sekta za uchumi usio rasmi au katika biashara ndogondogo, ndogo na za kati, ambazo huajiri idadi kubwa ya wanawake na vijana.  

“Janga hili ni mshtuko mkubwa kwa uchumi ulioendelea, lakini kwa nchi zinazoendelea ni dharura, haswa kwa nchi nyingi ndogo za visiwani zinazoendelea na nchi za Afrika. Kwa wanawake, jamii za vijijini, watu asilia na watu wengine wengi waliotengwa kihistoria, utalii umekuwa chombo cha kuwaunganisha, kuwawezesha na kutengeneza kipato. Utalii pia ni nguzo muhimu kwa uhifadhi wa urithi wa asili na kitamaduni.” Anasisitiza Bwana Guterres. 

Tweet URL

 

Ujangili umeongezeka 

Vilevile Bwana Guterres amesema kupungua kwa mapato kumesababisha kuongezeka kwa ujangili na uharibifu wa makazi ya viumbe na kuzunguka maeneo yaliyotengwa, na kufungwa kwa sehemu nyingi za urithi wa dunia kumeinyima jamii riziki. 

“Ni muhimu kwamba tuijenge tena sekta ya utalii. Lakini lazima iwe katika njia iliyo salama, sawa na rafiki kwa tabianchi.” Ameshauri Bwana Guterres. 

Pia ameeleza kuhusu uchafuzi wa hali ya hewa akieleza kuwa uzalishaji wa gesi ukaa itokanayo na usafirishaji unaweza kuongezeka tena ikiwa ari ya kusimama upya haitolinganishwa na malengo ya tabianchi. 

Guterres amesema kusaidia mamilioni ya watu ambao wanategemea utalii inamaanisha kujenga usafiri endelevu na wenye uwajibikaji ambao ni salama kwa jamii wenyeji, wafanyakazi na wasafiri. 

Ushauri ili kuokoa hali 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, baada ya kueleza namna ambavyo COVID-19 imeuathiri utalii kote duniani ameeleza maeneo matano ambayo ameyaanisha kuwa ni maeneo ya kipaumbele ili kusaidia hali kurejea kusimama upya.  

“Kwanza, kupunguza athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na janga hili. Pili, kujenga ustahimilivu katika mnyororo wa thamani kwenye utalii.Tatu, kuongeza utumiaji wa teknolojia katika tasnia ya utalii. Nne, kukuza uendelevu na ukuaji imara. Na ya tano, kukuza ushirikiano ili kuwezesha utalii kusaidia zaidi Malengo ya Maendeleo Endelevu.Tuhakikishe utalii unarejea tena kwenye nafasi yake kama mtoaji wa ajira,kipato thabiti na ulinzi wa urithi wetu wa kitamaduni na asili.”