Wazazi wana wajibu wa kuzungumza wazi na watoto kuhusu ubaguzi:UNICEF

25 Agosti 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linasema mazungumzo na watoto kuhusu tatizo la ubaguzi na ubaguzi wa rangi si suala rahisi lakini ni ya lazima na ni jukumu la wazazi na walezi.

Kwa Mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika hilo la UNICEF hakuna njia au mkakati mmoja ambao unaweza kutumika na kila mtu kuhusu kukabili suala la ubaguzi wa rangi hasa kwa watoto. 

Lakini ushahidi uko bayana kwamba jinsi wazazi au walezi wanavyoanza kuzungumza mapema na watoto kuhusu suala hii inasaidia kwani utafiti huo umedhihirisha  kwamba watoto wafikapo umri wa miaka 5 wanaweza kuanza kuonyesha dalili za ubaguzi wa rangi na kulipuuza suala hili hakutowalinda watoto bali kutawacha katika misingi ya kibaguzi ambayo imetawala maisha ya dunia hivi sasa. 

Priyanka Pruthi mtayarishaji wa vipindi wa UNICEF ambaye ameshiriki utafiti huo anasema kuna mambo matatu ya kuzingatia mosi ni kuwafundisha watoto kukumbatia tofauti zao “Katika umri huu watoto huenda wakaanza kutambua na kutaja tofauti miongoni mwa watu wanaowaona. Kama mzazi una fursa ya kuweka msingi taratibu kuhusu mtazamo wao. Jaribu kutafuta njia za kumtambulisha mwanao katika tamaduni na watu tofauti wa rangi na jamii tofauti. Maingiliano hayo mapema na watu na makundi mengine yanasaidia kupunguza ubaguzi na kuchagiza urafiki.” Pili Priyanka anasema kuwa wazi mbele ya watoto ni suala muhimu sana ili kuhakikisha kwamba mtoto yuko huru kukuuliza maswali wakati wote na pia kuwahimiza kuja kwako kama mzazi wakati wowote wanapokuwa na swali.

Na mbali ya hayo usiepuke kuwa mkweli wanapouliza suala kama la tofauti za rangi na pia kuhakikisha unalizungumzia suala la ubaguzi wa rangi kama kitu ambacho si haki ili liingie katika akili ya mtoto.

Na tatu ni kujenga imani  “Kuwa na majadiliano ya kweli na ya wazi kuhusu ubaguzi wa rangi, tofauti na ujumuishwaji hujenga imani na watoto na huwachagiza kuja kwako na maswali na mambo yanayowatia hofu. Endapo wanakuona kama mtu wanayemwamini kwa ushauri, kuna uwezekano wa kujihusisha nawe zaidi katika mada hiyo.” Na mwisho utafiti unasema ni vizuri kutambua tofauti na kutumia lugha muafaka kwa watoto kulingana na umri wao kwani kwa watoto wa umri wa miaka 6 hadi 11 hupenda kuchunguza, na kuzungumzia wanavyojihisi wakati vijana barubaru ambao muda mwingi wanautumia katika mitandao ya kijamii mambo ni tofauti. 

Hivyo ni lazima kujadili nao kuhusu wanayosikia na kuona kwenye vyombo vya Habari, kujua wanachokijua kupanua wigo wa uelewa wao , kuwachagiza kuchukua hatua dhidi ya ubaguzi wa rangi na mzazi au mlezi kuwa mfano wa kuigwa kwao. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter