Mbio za Selous zachagiza uhifadhi wa mazingira na utalii

24 Agosti 2020

Nchini Tanzania, Umoja wa Mataifa umesema utaendelea kushirikianana serikali katika kuhifadhi mazingira sambamba na kuhakikisha kuwa uhifadhi huo unachangia katika kuongeza kipato kwa wananchi. 

Ni katika safu ya milima ya Uluguru inayounda tao la mashariki, ambako Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa  nchini Tanzania Zlatan Milišić na Mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP nchini humo Christine Musisi wameongoza washiriki wa mbio za nyika za Selous kwa mwaka 2020 zenye lengo la kuchagiza uhifadhi wa mazingira na uendelezaji wa utalii.

Katika mbio hizo za tarehe 22 mwezi huu wa Agosti, washiriki walipita katika milima na mabonde ya eneo hilo na kushuhudia maajabu yaliyomo katika eneo hilo ambapo Bwana Milišić amesema kuwa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira unakwenda sambamba na kufikia malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu na jumuishi.

Hata hivyo amesema pamoja na miradi ambayo Umoja wa Mataifa inasaidia katika mabonde ya mto Ruvu na Zigi bado chombo hicho kitaendelea kuhakikisha hakuna yeyote anaachwa nyuma katika harakati za kusaka maendeleo.

UNDP na Tanzania

Kwa upande wake Bi. Musisi amepongeza washindi wa mbio hizo huku akiongeza, “napenda pia kuwapongeza sana GOFIN Ventures na waandaji wote wa mbio hizi kwa kuchagua Morogoro kama sehemu ya kuhamasisha mazoezi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya afya zetu.  Najua kwamba hili ni eneo zuri la kushirikisha vijana katika kuiweka miili yao imara wakati pia wakihamasisha utunzaji wa mazingira.”

Amezungumzia pia ushirikiano thabiti wa UNDP na Wizara ya Maliasili na utalii nchini Tanzania, ushirikiano ambao amesema umedimu kwa zaidi ya miaka 10 kupitia miradi mbalimbali yenye lengo la kufanikisha uhifadhi endelevu wa mazingira na usimamizi wa bora wa ardhi.

Ametaja maeneo ya ushirikiano kuwa ni pamoja na uhifadhi na usimamizi wa misitu ya tao la mashariki nchini Tanzania kati ya mwaka 2005 hadi 2011.

Halikadhalika uhifadhi na usimamizi bora wa maeneo oevu katika bonde la mto Ruvu na Zigi.

“Kupitia hatua hizo kumeweza kuanzishwa kwa maeneo ya uhifadhi wa misitu kutoka maeneo 5 mwaka 2015 hadi maeneo 17 mwaka 2020 kwenye eneo la takribani ekari milioni 1,” amesema Bi, Musisi.

Mbio hizo zilizopatiwa hashtag Na Mimi Nimo,ziliandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo Umoja waMataifa na serikali ya Tanzania.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter