Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali lazima zijitahidi kuwasaidia waathirika wa ukatili wa imani na dini:UN

Msikiti wa zamani huko Mazar-e Sharif.
UNAMA / Jawad Jalail
Msikiti wa zamani huko Mazar-e Sharif.

Serikali lazima zijitahidi kuwasaidia waathirika wa ukatili wa imani na dini:UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamezitaka serikali kuongeza juhudi ili kuwasaidia waathirika wa ukatili unaotokana na misingi ya kidini na Imani.

Katika taarifa yao maalum kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya waathirika wa vitendo vya ukatili kwa misingi ya Imani na dini inayoadhimishwa leo Agosti 22, wataalam hao wameelezea hofu yao kutokana na kuongezeka kwa kasi wakati huu wa janga la corona au COVID-19 kwa vitendo vya kikatili na chuki inayoelekezwa kwa jamii za kidini ambazo mara nyingi zinachukuliwa kama tishio kwa usalama wa ummma na utaifa. 

Wataalam hao wa haki za binadamu wametoa wito kwa serikali zote “Kukabiliana na hali ya kutovumiliana, ubaguzi na ukatili dhidi ya watu kwa misingi ya dini zao au Imani zao na kuzitaka serikali kufanya juhudi kubwa kuwasaidia waathirika wa ukatili hui ili wajenge upya Maisha yao na kuishi kwa uhuru bila hofu ya matukio hayo katika siku za usoni.” 

Msaada kwa waathirika ni muhimu 

Wataalam hao wamesisitiza kuwa “nchi zinapaswa kutambua umuhimu wa kuwapa waathirika wa vitendo vya kikatili kwa misingi ya dini au Imani na watu wa familia zao, msaada unaotakiwa kwa kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.” 

Pia wamezitaka nchi kuanzisha mtazamo madhubuti na jumuishi wa kijamii wa kuzia vitendo hivyo ambao unajumuisha wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kijamii na jumuiya za kidini, katika kulinda na kusaidia watu ambao wameathirika na kutopata haki na kukosekana kwa hatua madhubuti za kuwalinda. 

Ujumbe wa wataalam hao umeendelea kusema kwamba “ Tunatiwa wasiwasi na kuendelea kwa ubaguzi na ukatili kwa misingi au kwa kutumia jina la dini au Imani, ambao unawaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake na wasichana, watu walio kwenye makundi ya kidini, makabilia na makundi ya walio wachache, wasio amini au watu binafsi wenye mitazamo tofauti ya kidini au kisiasa, watu wa asili, watu wa LGBT Pamoja na wahamiaji na wakimbizi. Pia tunatambua kwamba watu walio katika kundi la wengi kwenye jamii pia wanakabiliwa na vitendo vya ukatili kwa misingo ya dini au Imani kutoka kwa wasio wafuasi wa serikali na ukandamizaji wa serikali.” 

Ongezeko la chuki 

Kwa mujibu wa wataalam hao wa haki za binadamu kunashuhudiwa ongezeko la chuki likielekezwa katika jamii tofauti za kidini wakati wa janga la COVID-19 , ukiwemo mwenendo unaotia hofu wa chuki dhidi ya Wayahudi. 

Wameongeza kuwa walio wachache na watu wanaokabiliwa na ubaguzi wa sehemu mara nyingi wanachukuliwa vibaya kwamba wanaathiri maingiliano ya kijamii au ni tishio kwa usalama wa umma na utaifa na mara kwa mara wanakabiliwa na vitendo vya kikatili. 

“Tunahofia kwamba serikali huenda zikatumia dini kama njia ya kushinikiza mitazamo finyu ya utaifa au kukiuka haki zingine za binadamu na usawa wa kijinsia. Hili sio tu kwamba linasambaratisha hadi ya kitaifa bali pia linachagiza ubinafsi badala ya kuchagiza kuheshimu utangamano na ujumuishaji.” 

Wameonya kwamba mwenendo huu umeochochewa zaidi na kutoheshimu haki ya uhuru wa dini na imani katika sehemu nyingi duniani. 

“Tunatoa wito kwamba uhuru wa dini au Imani umuhakikishie kila mtu haki ya kuchagua dini au imani, ikiwemo haki ya mtu kubadili dini au imani yake ya sasa.” 

Wamesisitiza kwamba uhuru wa dini na imani na haki zingine zote za binadamu kama vile haki ya uhuru wa maoni na kujieleza na haki ya kukusanyika kwa amani,  ni haki huru zinazoingiliana na kusisitiza ubinadamu, kwa misingi ya dini au Imani kwa kuwalinda watu dhidi ya chuki , ubaguzi na ukatili.