Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imevuruga harakati za kukabiliana na ugaidi- Guterres  

Nigeel kutoka Kenya anaongelea jinsi alikua bila baba yake ambaye aliuawa katika shambulio la Ubalozi wa Marekani mnamo 1998 iliathiri maisha yake.
UNCCT
Nigeel kutoka Kenya anaongelea jinsi alikua bila baba yake ambaye aliuawa katika shambulio la Ubalozi wa Marekani mnamo 1998 iliathiri maisha yake.

COVID-19 imevuruga harakati za kukabiliana na ugaidi- Guterres  

Amani na Usalama

Leo ni siku ya kimataifa ya kukumbuka waathiriwa na manusura wa vitendo vya kigaidi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema janga la COVID-19 linakwamisha harakati za kusaidia manusura wa ugaidi.  

Amesema huduma muhimu kama vile za kusaka haki kisheria na usaidizi wa kisaikolojia zimevurugwa, halikadhalika misada iliyokuwa inatoka serikalini kwa ajili yao imeelekezwa katika kupambana na janga la Corona. 

Kubwa zaidi ni kuahirishwa kwa matukio ya kukutana na kujadili tatizo la ugaidi, matukio ambayo huwa fursa kwa manusura kupata faraja na kwamba mkutano wa kwanza kabisa wa Umoja wa Mataifa wa manusura wa ugaidi umeahirishwa hadi mwakani. 

Bwana Guterres amesema kuwakumbuka manusura na kuwapatia msaada ni muhimu katika kuwawezesha kuondokana na msongo wa mawazo wa yale waliyopitia. 

Katika kufahamu janga la COVID-19 limeathiri vipi harakati za kusaidia manusura wa ugaidi, tumemuuliza James Ndeda, Mkurugenzi wa shirika la kiraia nchini Kenya la kusaidia manusura wa ugaidi, VITOK akisema kuwa, “tangu kutangazwa kwa janga la Corona, mikakati mingi ilisitishwa kwa sababu sheria ya nchi ikawa ni kwamba hakuna kukutana zaidi ya watu 15. Kumekuwa na kipindi ambacho watu walizuiwa kwenda sehemu mbalimbali ama kuingia katika sehemu mbalimbali, kwa mfano katika jiji la Nairobi watu walikuwa wamezuiwa kutoka ama kuingia katika jiji hilo kwa sababu ya COVID-19. Kwa hiyo mikakati ya VITOK ilikwama kwa muda huo.” 

 

Lakini kando ya changamoto ya sasa, tumemuuliza Bwana Ndeda ambaye yeye mwenyewe ni manusura wa shambulio la kigaidi nchini Kenya mwaka 1998 iwapo  anaona kuna fursa yoyote ya kusongesha harakati za VITOK?  

 

Bwana Ndeda amesema ni dhahiri kwa kuwa, “VITOK iko na fursa nyingi ya kuendeleza harakati zake kwa sababu ni shirika ambalo kwanza limesajiliwa na kukubalika na serikali ya Kenya. Ni shirika ambalo kando ya ujuzi hapa nchini wa kuendeleza mikakati yake, wanafanya kazi pia na mashirika ya kimataifa.” 

 

Hata hivyo Bwana Ndeda amesihi wadau wa kitaifa na kimataifa wasaidie katika kulipa fidia manusura sambamba na harakati zao za kuelimisha umma kuhusu madhara ya ugaidi.