Waliopindua nchi Mali lazima wamwachilie Rais Keita na kurejesha utawala wa sheria:UN

20 Agosti 2020

Mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mali leo amesema waliofanya mapinduzi nchini humo ni lazima wamwachilie Rais Ibrahim Boubacar Keita, waheshimu haki za binadamu na kurejesha utawala wa sheria. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mtaalam huyo huru kwa ajili ya haki za binadamu Mali Alioune Tine, amelaani vikali kukamatwa na kuwekwa rumande kwa Rais Keita katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Agosti 18 na kutoa wito wa viongozi wa mapinduzi kumuachia mara moja Rais huyo Pamoja na wajumbe wengine wa serikali yake na kulinda maisha yao na utu wao pamoja na familia zao. “Natoa wito kwa wajumbe wa kamati ya kitaifa ya ukombozi wa watu (CNSP) kukomesha mara moja kuwashikilia watu hawa kiharamu. Pia natoa wito kwa mamlaka zote za Mali kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa msingi, kuhamishia madaraka kwa raia haraka iwezekanavyo, kurejesha utawala wa sheria na kuhakikisha ulinzi wa mali na watu.” 

Waliokiuka haki wawajibishwe 

Mtaalam huyo pia ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti kwamba watu wane wameuawa na jeshi la ulinzi na wengine 15 kujeruhiwa usiku wa Agosti 18. 

Ametaka wote waliohusika katika ukiukwaji huo wa haki za binadamu kuwajibishwa na mamlaka za mfumo wa sheria wa Mali. 

Amesisitiza kwamba ni muhimu kwamba mapinduzi haya yamaeanzia kwenye mji wa Kati karibu na mji mkuu wa Mali Bamako, kama ilivyofanyika kwenye mapinduzi ya Machi 2012 ambayo yaliangusha utawala wa Amadou Toumani Touré ambayo yalizusha mgogoro unaondelea hadi leo. “Hili linapaswa kuyaamsha mataifa yote na wadau wa kimataifa kutafakari ni kwa jinsi gani waimarishe mifumo ya serikali ili tusirejee migogoro hii ambayo inasababisha kuendelea kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kupitia mgongo wa migogoro ya ndani ya jamii na baina ya jamii.” Ameongeza mtaalam huyo. 

Tine amekaribisha juhudi za jumuiya ya kiuchumi yan chi za Afrika Magharibi ECOWAS, na jumuiya ya kimataifa ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusaka suluhu ya amani ya kisiasa kwa mgogoro wa Mali, lakini amesema mfumo unapaswa kuimarishwa ili kuzuia , kudhibito na kutatua migogoro kama hii Afrika Magharibi. “Natoa wito kwa kila mtu nchini Mali, viongozi wa kisiasa, kijeshi na asasi za kiraia kujizuia na kujihusisha na majadiliano ya kina ili kurejesha amani ya kudumu, utulivu na kuheshimu haki za binadamu na uhuru mwingine wa msingi nchini Mali.”amekamilisha mtaalam huyo. 

Kwa sasa hali ni shwari 

Nao mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA leo umesema hali kwa sasa ni shwari, kuna utulivu ingawa bado Rais wa nchi hiyo na baadhi ya wajumbe wa serikali wanashikiliwa. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric kwa njia ya video mjini New York Marekani amesema msimamo wa Umoja wa Mataifa upo palepale kuheshimu haki za binadamu, kudumisha usalama na kuhakikisha mgogoro unatatuliwa kwa njia ya amani ya majadiliano ya kisiasa. 

Kwa mujibu wa MINUSMA ingawa huduma kubwa kama benki bado zimefungwa lakini maduka ya kawaida na masoko ya chakula yamefunguliwa ili kuhakikisha watu wanapata mahitaji ya lazima. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter