Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumedhamiria kupunguza pengo la kijinsia katika tasnia ya upigaji picha Tanzania-Nsamila

Imani Nsamila (wa nne nyuma kutoka kushoto) akiwa na kundi la wasichana waliohudhuria warsha ya upigaji picha.
UN/Imani Nsamila
Imani Nsamila (wa nne nyuma kutoka kushoto) akiwa na kundi la wasichana waliohudhuria warsha ya upigaji picha.

Tumedhamiria kupunguza pengo la kijinsia katika tasnia ya upigaji picha Tanzania-Nsamila

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania, mpiga picha maarufu, Imani Nsamila, kwa kushirikiana na shirika la Ladies Joint Forum na Kikoi innovative media, wamewapa mafunzo ya upigaji picha wasichana 28 ikiwa ni moja ya harakati za kuchangiakuyafikia malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu, SDGs, kama vile lengo namba 5 linalolenga ulimwengu kuwa na usawa wa kijinsia kufikia mwaka 2030. 

Imani Nsamila alisukumwa na nini kulilenga kundi hili? 

"Nilipofanya maamuzi kwamba naanza na kundi la aina gani kwanza nikaona ni bora nianze na kundi la wanawake kwasababu ni kundi ambalo watu wake wako wachache kwenye kiwanda hiki cha upigaji picha. Na pia mimi changamoto ninazozipata kwenye kazi mara nyingine naambiwa tunahitaji tupate mpigapicha wa kike ndio afanye jambo fulani sana sana watu ambao wana dini sana,hata kwa mfano kwa mambo ya harusi au 'kitchen party' wanapenda sana mtu ambaye anapiga picha awe mtoto wa kike kwa vile hiyo ni shughuli ya wanawake wanajihisi hawajatosheleka wakiwa na mpigaji picha wa kiume  na pia vitu vingi tu amabavyo vimenisukuma kusema nitaanza na kundi la watoto wa kike kwanza, labda baadaye naweza nikaleta hao wengine ambao kwa soko naona wako wengi"

Wasichana wakisikiliza kwa makini mafunzo ya upigaji picha yaliyoandaliwa na Imani Nsamila jijini Dar es salaam Tanzania.
UN/Imani Nsamila
Wasichana wakisikiliza kwa makini mafunzo ya upigaji picha yaliyoandaliwa na Imani Nsamila jijini Dar es salaam Tanzania.

 

Na je mpiga picha huyu anayesifika kwa kupiga picha zinazolenga kukuza uelewa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu ana mipango gani kwa siku zijazo baada ya warsha ya kwanza kufanikiwa? 

"Kwa mimi ninapofanya jambo hili imani yangu ni kwamba itabadilisha maisha yao kwa sababu katika dunia ya leo fursa yoteyote ambayo unaipata ya kuongeza elimu yoyote inachangia katika kubadilisha maisha yako hata watu unaokutana nao. Kwa hivyo mimi ninaamini kwamba elimu tuliyowapatia itakuwa ni chachu ya kubadilisha maisha yao kwa njia moja au nyingine. Nina imani kwamba wote watakuwa wapiga picha kwa vile nimewahamasisha na pia kuwa sehemu ya kubadili maisha yao.  Mpango mkuu wa kwanza ni kupunguza pengo ambalo lipo kati ya wapiga picha wa kiume na wa kike wa hapa Tanzania. Mpango wa pili ni kuwafikia mabinti wengi zaidi hapa Tanzania ikiwezekana Afrika nzima. Na mpango wa watu ni kwamba tunaanzisha mahali ama ofisi maalum ya wapiga picha. Mahali ambapo wapiga picha wote tutakutana na pia kushiriki katika kupeana mawazo. Kwa hivyo hii ndio inayofuata lakini baada ya hapo tutaweka muda kama miezi sita hivi kwa mfano wewe ukishakuwa umenufaika unamwachia na mwenzako naye aje anufaike na ambacho wewe umekipata ili tuwafikie watu wengi zaidi."