Mapinduzi ya kijeshi Mali, UN yazungumza

18 Agosti 2020

Kufuatia taarifa za mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa taarifa yake akisema kuwa anafuatilia kwa karibu kinachoendelea kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi.

Taarifa ya msemaij wake iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema kuwa “Guterres anafuatilia na wasiwasi mkubwa kile kinachoendelea Mali, ikiwemo kuasi kwa jeshi kulikotamatika kwa kukamatwa kwa Rais Ibrahim Boubacar Keita na viongozi kadhaa wa serikali yake mapema leo.”

Katibu Mkuu amelaani vikali vitendo hivyo na kutaka kurejeshwa haraka kwa utawala wa kikatiba na kisheria nchini Mali.

Amesema “kumaliza hili nasihi kuachiliwa huru bila masharti yoyote kwa Rais Keïta na mawaziri wake.”

Katibu Mkuu amesisitiza wito wake wa mashauriano na suluhu ya amani ili kumaliza tofauti zozote zilizopo.

Ameeleza kuwa anaung amkono juhudi za Muungano wa Afrika na Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS katika kusaka suluhu ya kudumu na kwa amani nchini Mali  ikiwemo kupitia kwa ofisi za mwakilishi wake maalum kwa Afrika Magharibi, UNOWA.

Halikadhalika amesihi wadau wote hususan vikosi vya ulinzi na usalama vijizuie kwa kiasi kikubwa na kuzingatia haki za binadamu na uhuru wa raia  wote wa Mali.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter