Machafuko yanayoendelea yawafungashaa virago watu milioni 1 Burkina Faso:UNHCR

18 Agosti 2020

Machafuko yanayoendelea kushika kasi nchini Burkina Faso sasa yamewalazimisha zaidi ya watu milioni moja kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo kwa njia ya video mjini Geneva Uswisi, msemaji wa shirika hilo Babar Baloch amesema tangu kuanza kwa mwaka huu pekee watu 453,000 wamekimbia makwao kwenda kusaka usalama na asilimia tano ya watu wote wa nchi hiyo sawa na mtu 1 kati ya 20 hivi sasa wametawanywa katika mgogoro huo wa kibinadamu unaokuwa kwa kasi kubwa. 

UNHCR inasema mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha Kaskazini na Mashariki mwa nchi hiyo yamewafanya watu kuhama mara nyingi na idadi ya wanaokimbia inatarajiwa kuongezeka zaidi, na majimbo mawili ya Burkina Faso ya Centre Nord na Sahel ndio yanayohifadhi asilimia sabini na sita 76 ya wakimbizi wote wa ndani. 

Kwa mujibu wa UNHCR mbali ya machafuko sasa janga la corona au COVID-19 limezidisha shida kwa watu wanaokimbia vita, machafuko na mauaji.

Jamii zinazowapokea zinahitaji haraka huduma muhimu za malazi, chakula, maji, ulinzi, afya na elimu hasa ukizingatia kwamba shule zaidi ya 2,500 zimelazimika kufungwa baada ya kulengwa na mashambulizi na hivyo kuwaacha wanafunzi   350,000 bila masomo. 

Kwa kushirikiana na serikali UNHCR inajiandaa kuhamisha idadi kubwa ya wakimbizi na kuwapeleka kwenye maeneo salama ambako huduma za msingi zinaweza kutolewa.

Na ili kutimiza mahitaji ya mamilioni ya watu Sahel, mwezi Juni mwaka huu UNHCR ilitoa ombi la dola milioni 186 kwa ajili ya kufikisha msaada wa kuokoa maisha kwa wakimbizi, wakimbizi wa ndani na jamii zinazowapokea katika nchi za Burkina Faso, Mali na Niger, ombi ambalo hadi sasa limefadhiliwa asilimia 53 tu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud