Kuendeleza huduma za msingi Sudan Kusini ni muhimu katika mapambano ya COVID-19:UNICEF

17 Agosti 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limesema muendelezo wa huduma za msingi zikiwemo chanjo kwa watoto Sudan Kusini ni muhimu sana katika vita dhidi ya janga la corona au COVID-19 na maradhi mengine.

Kwa mujibu wa UNICEF, nchini  Sudan Kusini asilimia 60 ya watu wanakosa huduma ya maji safi, watoto milioni 1.3 wataugua utapiamlo na kiwango cha chanjo hivi sasa ni asilimia 40 tu.  

Shirika hilo limeonya kwamba watoto wengi wako hatarini na kushughulikia mahitaji yao ya msingi ni muhimu sana ili kuwawezesha kuishi wakati huu wa janga la COVID-19, kwani hatua za kupambana na gonjwa hilo zimepunguza fursa za huduma na kuwema uhai wao njiapanda. 

Shirika hilo linasema watoto wengi wanakosa chanjo za msingi,  shule zimefungwa na wengi wako katika hatari ya ukatili na unyanyasaji. 

Licha ya changamoto hizo UNICEF na wadau wake wanajitahidi kuendelea kutoa huduma za kuokoa maisha na hadi kufikia sasa mwaka huu pekee watoto 292,000 wamepatiwa chanjo ya surau na milioni 1.6 wamepewa matone ya vitamin A. 

Mbali ya chanjo, UNICEF imetoa msaada wa kisaikolojia kwa wavulana na wasichana 13,000 nchini humo na watoto wengine zaidi ya laki moja wamepata matibabu dhidi ya utapiamlo. 

Katika kupambana na malaria shirika hilo limeshagawa wajawazito na watoto vyandarua 148,000 vya ya kujikinga na mbu.

Na kupambana na maambukizi ya COVID-19 UNICEF imehakikisha watu wengine 260,000 wamepata huduma ya maji safi na salama.  

Shirika hilo limeahidi kuendelea kufanya kila juhududi kuhakikisha maisha ya mamilioni ya watoto wa Sudan Kusini yanaokolewa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter