Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tamasha la aina yake lafanyika kuunganisha ukanda wa Pasifiki dhidi ya COVID-19

Ngoma ya utamaduni kutoka Fiji ikichezwa wakati wa tamasha hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao
UN Web TV Screenshot
Ngoma ya utamaduni kutoka Fiji ikichezwa wakati wa tamasha hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao

Tamasha la aina yake lafanyika kuunganisha ukanda wa Pasifiki dhidi ya COVID-19

Afya

Tamasha la kwanza la aina yake kuwahi kufanyika kwa njia ya televisheni na mtandao kuhusu harakati za ukanda wa Pasifiki kuungana, Pacific Unite limefanyika leo likitoa wito kwa viongozi na wakazi wa ukanda huo kuungana ili kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa, wasanii na watu mashuhuri duniani wameshiriki tamasha hilo likiwa ni la kwanza la kikanda kusongesha harakati dhidi ya COVID-19.

"Ninajivunia sana kuwa sehemu ya tukio hili la kihistoria," amesema Tofiga Fepulea’i, ambaye ndiye aliandaa tamasha hilo akisema kuwa, "sasa ni wakati wa sisi kuwa pamoja na kusherehekea uthabiti wet una suluhu ambazo zinaweza kupatikana pindi ukanda wa Pasifiki unapoungana."

Tamasha hilo la saa mbili na nusu limeleta pamoja wanamuziki kutoka mataifa 12 ya visiwani Pasifii wakiwemo Jahboy kutoka visiwa vya Solomoni, Mia Kami wa Tonga, Juny B wa Kiribati, Te Vaka wa New Zealand na wengine wengi.

Halikadhalika kulikuwepo na ujumbe kwa njia za video kutoka wageni wa kimataifa akiwemo Prince Charles wa Uingereza, mchechemuzi wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, Forest Whitaker ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Oscar na pia muigizaji mashuhuri kutoka Marekani. Wengine ni Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern.

Mshikamano

Tamasha hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao na kurushwa na vituo vya televisheni na pia mtandaoni lilikuw ni jukwaa la kuwaunganisha watu wa Pasifiki ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amesisitiza ujumbe wa mshikamano kama njia pekee ya kutokomeza COVID-19.

Watumbuizaji wakiimba wakati wa tamasha hilo la kuunganisha visiwa vya Pasifiki dhidi ya COVID-19
UN Web TV Screenshot
Watumbuizaji wakiimba wakati wa tamasha hilo la kuunganisha visiwa vya Pasifiki dhidi ya COVID-19

"Bado kuna mengi hayajafanyika na hakuna mtu au nchi inaweza kufanya peke yake," amesema Bi. Mohammed katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameangazia wajibu wa jamii ya kimataifa kufanya kazi pamoja kusaidia kile alichosema ni "majirani zetu wa visiwa vidogo" katika kukabili janga la Corona kwa kuhakikisha kuwa nao wanapata vifaa muhimu vya tiba na pindi itakapopatikana chanjo, nayo pia wapatiwe.

Amesema kuwa jamii ya kimataifa nayo inapaswa kusaidia chumi za nchi za visiwa vidogo kupitia misamaha ya madeni na misaada ya haraka inayochochea uchumi jumuishi na wenye mnepo.

"Hebu na tusimame pamoja kukabili hivi virusi. Hebu na tusema hapa kwa ghasia, hapana kwa ubaguzi, hapana kwa unyanyapaa, hapana kwa taarifa za uongo," amesema Bi. Mohammed huku akiongeza kuwa, "hebu na tuseme ndio kwa mshikamano, ndio kwa upendo, ndio kwa kuhudumiana kwa mfumo wa kipasifiki."

Madhara kwa mapana

Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.
UNDP Tuvalu/Aurélia Rusek
Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.

Tayari COVID-19 imekuwa na madhara makubwa kwa nchi za visiwa hivyo vya Pasifki ambapo utalii umetwama, biashara ya kimataifa halikadhalika kiwango cha fedha kinachotumwa katika nchi hizo kimepungua.

Halikadhalika kupitia tamasha hilo la muziki, kumeibuliwa masuala kama ukatili wa majumbani, ukosefu wa ajira, ukosefu wa chakula na tatizo la afya ya akili, vyote vikichochewa na COVID-19.

Wazungumzaji wamesisitiza umuhimu wa kujenga upya mataifa hayo na kwa njia endelevu zaidi ili ukanda huo uwe na mnepo pia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Hii kawaida mpya haipaswi kuwa simulizi ile ile ya zamani, lakini sambamba na barakoa," amesema Rais wa visiwa vya Palau, Tommy E. Remengesau Jr, kupitia ujumbe wake kwa njia ya video.

Amesema visiwa vya Pasifiki vimekuwa vikichukua hatua kubwa za mabadiliko kwenye sekta ya utalii, uvuvi, matumizi ya plastiki na uzalishaji wa nishati na kwamba kwa njia ya ajabu, COVID-19 imefungua njia ya kufikia malengo hayo.

"Iwapo tunaweza kukabili changamoto hii kwa njia sahihi, basi tunaweza kujenga mfumo thabiti zaidi kuliko awali," amesema Rais huyo wa Palau.

Tukio la mwisho

Tamasha lilitamatishwa na wimbo maalum uitwao We Will Rise, au tutanyayuka! Ulioandikwa kuhusu virusi vya Corona ukanda wa Pasifiki na ukatumbuizwa na Pasifika Voices na shule ya kimataifa ya Suva.