Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa ombi la dola milioni 565 kuisaidia Lebanon baada ya mlipuko

Bandari ya Beirut baada ya mlipuko
Houssam Yaacoub
Bandari ya Beirut baada ya mlipuko

UN yatoa ombi la dola milioni 565 kuisaidia Lebanon baada ya mlipuko

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa leo umezindua ombi la dola milioni 565 ili kuwasaidia watu wa Lebanon kutoka katika msaada wa dharura wa kibinadamu wa kuokoa Maisha na kuingia katika hatua ya kujikwamua na ujenzi mpya na hatimaye kuelekea katika hatua za muda mrefu za kujikomboa kiuchumi kufuatia milipuko ya wiki iliyopita katika bandari ya Beirut.

Katika taarifa ya ombi hilo Umoja wa Mataifa umesema milipuko iliyotokea Agosti 4 kwenye bandari ya Beirut imesambaratisha asilimia kubwa ya bandari hiyo, maeneo jirani na kuharibu hospitali 6 na kliniki za afya zaidi ya 20.  Pia watu zaidi ya 6,500 wamejeruhiwa na maelfu kuachwa bila makazi. 

Matumizi ya fedha hizo 

Fedha hizo zikipatika zitawawezesha wadau wa misaada ya kibinadamu kuwasaidia watu wenye mahitaji ya muhimu hasa yakilenga:

Mosi uhakika wa chakula kwa kuhakikisha haraka chakula kilicho tayari kinatolewa sambamba na mgao wa chakula na usambazaji wake.  

Pili afya kwa kukarabati kwa vituo vya afya na kutoa matibabu ya wagonjwa mahututi na dawa zingine muhimu. 

Tatu, malazi kwa kutoa fedha kwa ajili ya malazi kwa familia ambazo zimehamishwa kutokana na kuharibiwa au kusambaratishwa kabisa kwa nyumba zao na kulipia ukarabati wa maeneo na majengo ya umma ambayo yaliathirika na mlipuko na pia suala la ulinzi pamoja na kusaidia huduma za maji na usafi. 

Mlipuko katika bandari ya Beirut ulisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya makazi
© UNOCHA
Mlipuko katika bandari ya Beirut ulisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya makazi

Naibu mratibu maalum kwa ajili ya Lebanon na mratibu wa masuala ya kibinadamu Najat Rochdi amesema “Kiwango cha hasara kutokana na mlipuko wa Beirut ni kubwa sana na kuna uwezekano kila mtu Lebanon ameguswa na janga hilo. Nimeshuhudia uharibifu mkubwa na hofu iliyotanda , lakini pia nimejionea mnepo mkubwa na utu wa watu wa Lebanon ambao wamejitokeza kusaidiana kwa upendo na huruma.” 

Ameongeza kuwa kazi ya kujenga upya maisha ya watu na kujikwamua kutoka kwa athari za janga hilo ndio kwanza zinaanza. “Naiomba jumuiya ya kimataifa kuonyesha na kutimiza ahadi zao kwa watu wa Lebanon na kulipa fadhila kwa ukarimu mkubwa wa watu wa Lebanon wanaoutoa kwa wakimbizi wa Syria na Palestina kwa kuwasaidia kikamilifu na fedha zinazohitajika” Amesema mratibu huyo wa masuala ya kibinadamu Lebanon.