Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yashikamana kukidhi mahitaji ya waathirika wa mlipuko Beirut

Wafanyikazi wa WFP wakiwa nchini Lebanon
WFP/Malak Jaafar
Wafanyikazi wa WFP wakiwa nchini Lebanon

Mashirika ya UN yashikamana kukidhi mahitaji ya waathirika wa mlipuko Beirut

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kujikusanya na kugawa misaada ili kukidhi mahitaji ya waathirika wa mlipuko mjini Beirut.  Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP hivi sasa linajiandaa kusafirisha maelfu ya tani za unga wa ngano ili kujaza ghala la chakula cha msaada lililosambaratishwa na mlipuko huo kwenye bandari ya Beirut. 

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya video mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema “WFP iko Beirut kukidhi mahitaji ya dharura na ya muda mrefu ya chakula na hasa kwa watu walio hatarini zaidi nchini Lebanon.” 

Awamu ya kwanza ya shehena ya uga wa ngano inatarajiwa kuwasili kwenye bandari ya Beirut Agosti 20 mwaka huu na msaada huo utagawiwa mara moja kusaidia maduka ya kuoka mikate  na kisha ngano ambayo bado haijasagwa itapelekwa kwenye vinu vya kusaigia katika maeneo jirani. 

Msaada mwingine wa WFP 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limeandaa vifurushi 150,000 vya chakula ambavyo litavigawa kwa familia zilizoathirika na mgogoro wa kiuchumi na pia hatua za kupambana na COVID-19. 

Zaidi ya hapo litaongeza mara kumi msaada wa program yake ya kugawa fedha taslim ili kuwasaidia watu milioni moja wakiwemo wakazi walioathirika moja kwa moja na mlipuko huo. 

Hatua zote hizi kwa mujibu wa WFP ni sehemu ya operesheni ya haraka ambayo inahusisha kujenga maghala na vituo vya kuhifadhi nafaka. “Ni muhimu kwamba sehemu ya bandari ikakarabatiwa na kurejea kufanya kazi haraka iwezekanavyo” ameongeza bi Byrs. 

Msaada wa WFP kwa Lebanon
WFP/Ziad Rizkallah
Msaada wa WFP kwa Lebanon

 

Timu ya Umoja wa Mataifa inafanya kazi kubwa hivi sasa ya kukarabati sehemu muhimu ya bandari hiyo na WFP wiki hii itasafirisha mahitaji kwa njia ya ndege ili kuhakikisha bandari hiyo inafanyakazi ipasavyo ili kusaidia uingizaji wa kiwango kikubwa cha ngano na nafaka zingine nchini Lebanon. 

Hata hivyo shirika hilo limesema msaada huu wa dharura iliouzindua nchini Lebanon unahitaji jumla ya dola milioni 235 kwa ajili ya kuwezesha kutoa msaada wa chakula kwa watu wasiojiweza na walio hatarini kwa kipindi cha miezi sita , lakini pia msaada wa kiufundi na kusaidia usambazaji wa chakula nchini humo. 

Watu 30 bado hawajapatikana 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imetoa takwimu mpya kufuatia mlipuko huo wa wiki iliyopita Beirut na kusema kwamba hadi kufikia sasa idadi ya waliopoteza Maisha imeongezeka na kufikia 180, wengine 6000 walijeruhiwa na angalao watu 30 bado hawajapatikana. 

Katika tathimini yake iliyotolewa jana OCHA imesema mlipuko huo mkubwa wa Beirut umeathiri operesheni za hospitali 6 na pia kuharibu kliniki zaidi ya 20. "Tathimini ya awali iliyofanyika katika eneo la kilomita 15 kutoka kwenye mlipuko imebaini kwamba katika jumla ya vituo vya afya 55 ni nusu yake tu ndio vinavyofanya kazi kikamilifu na karibu asilimia 40 vimeharibiwa kwa kiasi fulani na vinahitaji ukarabati.” 

Shule 120 ambazo zinahudhuriwa na watoto 50,000 zimeharibiwa nyumba zaidi ya 1000 kati ya nyumba 50,000  zimeharibiwa vibaya imesema ripoti hiyo ya OCHA. 

Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.
© UNOCHA
Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.

Fedha zahitajika ili kukidhi mahitaji 

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imebidi lifanyie marekebisho ombi lake la fedha ikiwa ni siku 10 tangu kutoa kwa mlipuko huo. 

Sasa linasema katika miezi mitatu ijayo litahitaji zaidi ya dola milioni 46 kuweza kuwasaidia Watoto 100,000 nchini Lebanon. 

Fedha hizo Pamoja na masuala mengine zitasaidia ukarabati wa vituo 16 vya afya ya msingi ambavyo vilikuwa vinatoa huduma kwa watu 160,000. Pia shirika hilo linasema ni muhimu kukarabati shule na kuhakikisha kwamba Watoto ambao nyumba ao zimebomolewa wanaendelea kusoma iwe ni darasani au kupitia elimu mtandaoni ambayo itakuwa imewekewa utaratibu wakati wa janga la COVID-19. UNICEF inaamini kwamba athari za muda mrefu za mlipuko huo kwa Watoto bado hazijafahamika vyema. “Athari zake zitakuwa ni za miezi na  hata miaka . Watoto wa Lebanon wanahitaji msaada wetu unaondelea, anastahili kila tuwezalo“ amesema naibu mwakilishi wa UNICEF  nchini Lebanon Violet Speek-Warnery. 

Udhibiti wa taka na kifusi 

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP limesema kitu cha haraka hivi sasa ni tathimini ya uharibifu wa nyumba na maduka katika maeneo yaliyoathirika na mlipuko huo. 

“Tunatathimini aina ya kifusi, matofali, nondo na vioo. Taka hatari, taka za kitabibu na taka za kielektroniki lazima zishughulikiwe vyema.” Amesema Rekha Das mshauri wa mgogoro na dharura wa UNDP. 

Ameongeza kuwa “Ni lazima tubaini nini kilicho hatari na kipi salama, nini kinaweza kurejelezwa na kipi hakifai. Lengo ni kubaini endapo taka hizi zinaweza kutupwa endapo haziwezi kurejelezwa.” 

Das amesema kwamba mbali ya taka na uchafuzi wa mazingira unaoonekana bayana , uchaguzi wa hewa na athari za kimazingira za mlipuko huo katika bahari ya Mediterranea hazijulikani. 

UNDP imeahidi kusaidia katika ujenzi mpya wa mji wa Beiruti kujikwamua kiuchumi hasa maeneo yaliyoathirika. “Tuna unda ajira, tutatoa ufadhili na mikopo ya fedha ili kuanzisha tena biashara ndogondogo naza wastani katika njia endelevu hususan kwa wanawake wengi ambao wamepoteza njia za kujikimu kuweza kuishi.” amesisitiza mshauri huyo wa UNDP.