Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya Israel na UAE ni kitu ambacho UN imekuwa inakipigia chepuo

Al- Walaja, kijiji cha kipalestina kwenye ukingo wa magharibi mwa Mto Jordan
© UNRWA/Marwan Baghdadi
Al- Walaja, kijiji cha kipalestina kwenye ukingo wa magharibi mwa Mto Jordan

Makubaliano ya Israel na UAE ni kitu ambacho UN imekuwa inakipigia chepuo

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema ya kwamba makubaliano yaliyofikiwa kuhusu Mashariki ya Kati, ni jambo ambalo Katibu Mkuu wa chombo hicho chenye wanachama 193 amekuwa akikipigia chepuo kila uchao.

Makubaliano hayo yenye lengo la kusitisha mpango wa upanuzi wa ujenzi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi kwenye eneo linalokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan yamefikiwa Alhamisi na kisha taarifa ya pamoja kutolewa na Rais Donald J. Trump wa Marekani, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mwanamfalme wa Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Zayed Al Nahyan.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Alhamisi usiku wa tarehe 13 Agosti mwaka 2020 punde baada ya makubaliano hayo, imemnukuu Bwana Guterres akisema kuwa, "nyongeza ya majengo ingalifunga milango ya mashauriano mapya na kusambaratisha matumaini ya uwepo wa taifa la Palestina na suluhu ya mataifa mawili kuwepo kwa wakati mmoja."

Mpalestina akiwa kwenye mitaa ya Hebron, kwenye Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan.
UNRWA/Marwan Baghdadi
Mpalestina akiwa kwenye mitaa ya Hebron, kwenye Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan.

Katibu Mkuu amekaribisha makubaliano hayo, "akitumai kuwa yatajenga fursa kwa viongozi wa Israel na Palestina kujadiliana kwa dhati ili hatimaye kufikia suluhu ya mataifa mawili yaani Palestina na Israel kuwepo sambamba kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano kati ya pande mbili hizo."

Katibu Mkuu amesema amani Mashariki ya Kati ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote katika eneo hilo hivi sasa wakati linakabiliana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 na uenezaji wa misimamo mikali.

Taarifa imesema kuwa Bwana Guterres anaendelea kufanya kazi na pande zote ili kufungua milango zaidi ya mazungumzo, amani na utulivu.

Vyombo vya habari vinaripoti ya kwamba makubaliano kati ya Israel na Falme za kiarabu ya kurejesha mahusiano yao, yanafuatia mazungumzo kwa njia ya simu baina ya viongozi wa Israel na Rais Trump wa Marekani na hivyo kufanya kuwa mkataba wa kwanza wa amani kati ya Israel na Falme za Kiarabu katika kipindi cha miaka 25.

Kupitia makubaliano hayo, Israel imekubali kusitisha mpango wake wa kupanua makazi ya walowezi huko Yudea na Samaria kwenye Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan na kufanikisha uhusiano na Falme za kiarabu na pia na nchi nyingine za kiarabu na kiislamu.