Watu 4 kati ya 10 nchini DRC hatarini kukosa chakula, msaada zaidi unahitajika- WFP

14 Agosti 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP hii leo mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC limeonya kuwa kutokana na hali ya mgogoro pamoja na virusi vya corona vinavyoendelea kuongezeka nchini humo DRC na hivyo kuzidisha moja ya janga kubwa la njaa duniani na ambalo linapata ufadhili mdogo, mamilioni ya watu wanaweza kupoteza maisha ikiwa jumuiya ya kimataifa haitaingilia kati na usaidizi zaidi. 

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, watu wanne kati ya kumi ya watu milioni 100 wa DRC waliokadiriwa, wako katika hali ya kukosa chakula huku watu milioni 15.6 wakiwa tayari wanakabiliwa na janga au dharura ya njaa.  

Mwakilishi wa WFP nchini DRC Claude Jibidar amesema, “raia wengi wa Congo wako ukingoni na hata katika hatari kubwa hivi sasa ya kuporomoka. Ulimwengu hauwezi kuacha hilo litokee, ingawa inaeleweka ni kuhusu ongezeko kubwa la COVID-19 linalochukua maisha na njia za kuishi mahali kwingine.” 

Ufadhili unahitajika 

WFP inahitaji dola milioni 172 nyingine, ili kuweza kutekeleza kikamilifu shughuli zake za dharura nchini DRC kwa miezi sita ijayo. Shirika hilo linapanga kuwasaidia watu milioni 8.6 kwa mwaka huu wakiwemo ongezeko la takribani watu milioni moja ambao wameathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona au COVID-19.

Shirika hilo linaongeza kuwa bila kupatikana kwa fedha zinazohitajika, mgao wa chakula na msaada wa fedha taslimu vitalazimika kusitishwa na hivyo kupungua kwa idadi ya watu wanaosaidiwa.  

“Shughuli za kutibu na kuzuia utapiamlo mkali ambao unaaathiri watoto wa DRC wapatao milioni 3.4 ziko hatarini.” Imesema taarifa ya WFP.  

Utapiamlo kwa watoto wa DRC unashuhudiwa hususani katika maeneo yenye vita, maeneo ya mashariki mwa DRC kwenye utajiri wa madini ambako miongo kadhaa ya mapigano ya kikatili na mapigano ya kikabila vimewalazimisha mamilioni ya raia kuyakimbia makazi yao, wengi wao wakikimbia mara kadhaa.   

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud