Watoto Haiti na uelewa wa kina jinsi ya kujikinga na COVID-19

14 Agosti 2020

Kampeni iliyoendeshwa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na Wizara ya Afya ya Umma na Idadi ya watu nchini Haiti kuhusu jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona, au COVID-19, imekuwa na mafanikio katika kupunguza maambukizi na hata watoto wana uelewa.

Katika mji wa Dame Marie nchini Haiti tunakutana na mtoto Wisphania Metellus mwenye umri wa miaka 11, akiwa na wenzake wanacheza mdako.  

Tangu kuibuka kwa COVID-19 nchini humo mwezi Machi mwaka huu, yeye na wenzake hawaendi shule kwa kuwa zimefungwa ili kupunguza maambukizi. “Kwa kuwa siendi shuleni, nabakia nyumbani na kufanya kazi za kila siku. Nafagia ua, nasafisha nyumba, natandika kitanda na kufagia jikoni," 

Wisphania anatambua kanuni za afya na amezishika kichwani hii ni kutokana na harakati za UNICEF na anasema, "Kujikinga na huu ugonjwa, lazima tusafishe mikono yetu mara kwa mara, hatushikani mikono, hatukumbatii watu na tunakaa umbali wa mita mbili kati ya mtu na mtu." 

UNICEF inasema kuwa kutambua kanuni za kujikinga na Corona kutasaidia kuokoa maisha ya maelfu ya watoto katika taifa hilo ambalo hadi sasa wagonjwa zaidi ya 7,700 wameugua Corona na kati yao hao 187 wamefariki dunia. 

Shirika hilo limehamasisha mashirika 15 ya kimataifa na kiraia nchini humo kuendesha kampeni za kuelimisha watu jinsi ya kujikinga na COVID-19 ambapo kila uchao wafanyakazi wa kujitolea wa kijamii wanachanja mbuga kufikia wale walio mbali zaidi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter