Restless Development imetuwezesha kuanzisha kiwanda cha chaki

Simon Philipo Sirilo, mnufaika wa miradi ya Restless Development nchini Tanzania.
Restless Development Tanzania
Simon Philipo Sirilo, mnufaika wa miradi ya Restless Development nchini Tanzania.

Restless Development imetuwezesha kuanzisha kiwanda cha chaki

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania, shirika la kiraia la Restless Development limekuwa mstari wa  mbele kuona vijana wanapata stadi mbali mbali muhimu ili hatimaye siyo tu wawe viongozi kwenye jamii zao bali pia waweze kushiriki shughuli za ujasiriamali na kunusuru vijana wenzao kutoka katika lindi la  Umaskini.

Miongoni mwao Simon Paul Cyrilo ambaye anasema katika mambo mengi aliyojifunza ni mawili tu ambayo yamegusa zaidi maisha yake, akisema ni, “jambo la kwanza ni suala zima la uongozi ambapo nilitumia maelekezo yote niliyopewa kama  sehemu ya mahojiano ambayo niilifanya na hatimaye mwaka jana nikafanikiwa kuingia katika nafasi ya uongozi wa kiserikali baada ya kupita kwenye mahojiano. Hata yote nasema ni msaada tosha kutoka shirika la Restless Development, jinsi walivyonielekeza ndivyo nilivyofanikiwa.” 

Mnufaika huyu anaenda mbali zaidi akigusia mradi mwingine wa ICS ulioko Restless Development kuhusu ujasiriamali akisema nao umekuwa na manufaa makubwa na, “ni msaada tosha katika maisha yangu ambapo hadi sasa licha ya kuwa kiongozi ninajihusisha na ujasiriamali. Nilijifunza mambo mengi ya ujasiriamali lakini nikasambaza elimu hiyo kupitia maandishi ambapo niliandika kitabu kiitwacho Mjasiriamali wa Leo Tajiri wa Kesho. Lakini pia shirika lilinisaidia kuniunganisha na Radio Kati FM iliyoko Iringa ambako nilifanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana kuhusu ujasiriamali.” 

Lakini Simon hakuwa mchoyo kwa kuwa, “nilipoingia mtaani, nilianza kuelimisha makundi mbalimbali, vijana, wanawake na wanaume. Llakini pia vijana walijifunza mambo mengi na nikawashauri tuunde vikundi na tulifanikiwa kuanzisha kikundi kilichopo wilaya ya Ikungi mkoani Singida, na tukaanzisha mradi mkubwa wa kutengeneza chaki, baadaye serikali ilituona na kutushika mkono na kututafutia soko katika wilaya ya Ikungi na mkoa wa Singida kwa jumla.”