Lazima haki na uwajibikaji vitendeke kufuatia mlipuko wa Beiruti:Wataalam UN

13 Agosti 2020

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamesema janga la mlipuko lililotokea Beirut Lebanon Agosti 4 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu wengi na kujeruhi wengine kwa maelfu, linahitaji uchunguzi huru na wa haraka ambao utazingatia wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu, utakaotanabaisha majukumu ya mlipuko huo na hatimaye kufikia kupata haki na uwajibikaji kwa wahusika. 

Kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Geneva Uswisi wataalam hao wamesema “kiwango na athari za mlipuko huo hazielezeki na si za kawaida. Tunatiwa hofu kubwa kuhusu kiwango cha kutowajibika na ukwepaji sheria dhidi ya athari za kibinadamu na mazingira zilizosababishwa na janga hilo. Mlipuko huo ulitokea wakati ambapo Lebanon tayari ilikuwa inakabiliwa na changamoto za kisiasa, uchumi na mgogoro wa kifedha lakini pia janga la corona au COVID-19 changamoto ambazo zimechangia kuzorota kwa ulinzi wa haki za binadamu na kuwasababishia watu wa nchi hiyo madhila makubwa.” 

Hali halisi 

Hadi kufikia sasa takriban watu 200 wamepoteza maisha, maelfu wamejeruhiwa na angalau watu 300,000 wameachwa bila makazi wakati juhudi zikiendelea kuwasaka mamia wasiojulikana waliko. 

Wataalam hao wamenya kwamba wakati bandari kuu ya Beiruti na magahala ya chakula ya nchi hiyo yaliwa karibu kusambaratika kabisa kutokana na mlipuko huo, ambao pia umeathiri hospitali na vifaa tiba kwa kiasi kikubwa uwezo wa malaka ya nchi hiyo kukidhi wajibu wao wa kulinda haki ya chakula, malazi na haki ya afya umeathirika vibaya. 

Na kwa sasa msaada wa haraka, kuwaunga mkono na kulipa fidia waathirika ni muhimu bila kubagua. Wataalam hao pia wametoa wito kwa mamlaka ya serikali kuruhusu maandamano ya amani na kuwalinda waandamanaji na waandishi wa Habari. 

Wamesisitiza kwamba “Walebanon wote, asasi za kiraia na jamii zilizoathirika wanapaswa kuweza kushawishi maamuzi ya serikali kwa uhuru katika kipindi hiki muhimu, ikiwemo katika masuala ya kuratibu, kusimamia na kusambaza misaada yoyote inayotoka nje.” 

Haki ya kujua kinachoendelea 

Wameongeza kuwa kila mtu nchini Lebanon ana haki ya kupata taarifa kuhusu hatari za kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na rundo la kemikali hatari zinazohifadhiwa nchini humo na taarifa kama hizo lazima ziwekwe wazi, zipatikane na zitolewe kwa njia ambayo ni ya muendelezo na kwa misingi isiyobagua.

Kwa mujibu wa duru za Habari hewa chafuzi iliyotolewa na mlipuko huo ni chanzo cha hewa mbaya na uchafuzi wa mazingira mjini Beirut, hivyo watu wote wana haki ya kujua hatari za kuvuta hewa hiyo yenye kemikali ya nitrous oxide na nyinginezo kwa afya zao. 

Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka za Lebanon kusaidia uokoaji na masuala mengine baada ya mlipuko mkubwa mjini Beirut uliosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.
UNOCHA
Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka za Lebanon kusaidia uokoaji na masuala mengine baada ya mlipuko mkubwa mjini Beirut uliosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.

Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuwapa kipaumbele maalum wazee, watu wenye ulemavu na wengine ambao wana mahitaji maalum na walioathirika zaidi na dharura hiyo. 

Wamesema chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na mazingira , nchi na makampuni ya biashara yana wajibu wa kuchukua hatua kukabiliana na hatari zinazosababishwa na kemikali hizo na kwamba serikali haiwezi kufumbia macho suala hilo. 

Wamesisitiza kwamba ni lazima wachukue hatua haraka na za kina kuzuia kupotea kwa maisha ya watu, changamoto za kiafya na athari za kimazingira.

Mlipuko waibua mengi 

Wataalam hao wamesema mlipuko huo na athari zake umeweka bayana matatizo ya kimfumo yaliyopo Lebanon ikiwemo ukosefu wa utawala bora na madai ya kusambaa kwa ufisadi hali ambayo imesababisha kushindwa kuhakikisha ulinzi wa haki kwa wote bila ubaguzi, ikiwemo haki ya kuishi, uhuru binafsi, afya, malazi, chakula, maji, elimu na mazingira yenye afya. 

“Tuna tiwa wasiwasi kwamba janga hili litaweka bayana nyufa zilizopo katika taasisi za utawala, sheria na haki, na hivyo kuchelewesha na kusababisha changamoto katika kuhakikisha huduma na haki inapatikana kwa wote walioathirika.” 

Wataalam hao wametaka uchunguzi pia uzingatie wajibu wa kimataifa wa Lebanon katika kushughulikia kemikali za hatari na haki ya kila mtu kupata taarifa kuhusu hatari kwa maisha na afya zao kutokana na kemikali hizo. Na mbali ya haki za binadamu na makosa ya jinai wametaka uchunguzi huo umulike kwa kina pia wajibu wa Lebanon chini ya sheria za kimataifa za biashara na usafirishaji wa bidhaa. 

Mwisho wamesema wako tayari kushirikiana na serikali ya Lebanon, asasi za kiraia na jumuiya ya kimataifa ikiwemo katika kusaidia uchunguzi na hatua zingine za kupunguza athari za janga hilo, kuhakikisha uwajibikaji, ujenzi mpya katika kuheshimu dini mbalimbali zinazojenga taifa hilo na kuzuia janga kama hilo kutokea tena. 

Pia wameitaka jumuiya ya kimataifa kutoa msaada kwa wakati kwa watu wote nchini Lebanon ikiwemo madai yao ya haki kwa misingi ya mshikamano na ushirikiano wa kimataifa. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter