Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kupeleka unga wa ngano na nafaka nchini Lebanon

Msaada wa WFP kwa Lebanon
WFP/Ziad Rizkallah
Msaada wa WFP kwa Lebanon

WFP kupeleka unga wa ngano na nafaka nchini Lebanon

Msaada wa Kibinadamu

Ili kusaidia kupambana na uhaba wa chakula nchini Lebanon baada ya mlipuko uliotokea tarehe 4 Agosti mwaka huu, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, linapeleka nchini humo unga wa ngano na nafaka katika kipindi hiki ambacho nchi inajenga upya bandari yake na imesaliwa na hifadhi ya unga wa ngano inayokadiriwa kukidhi mahitaji ya soko kwa kipindi cha wiki sita.

Ni picha na video za magofu ya mji wa Beirut uliosambaratishwa kwa sehemu kubwa, zinazoendelea kusambaa kote duniani. 

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP, David Beasley ambaye amefika hapa kujionea hali, anasema picha hazitoshi kuonesha ukweli halisi ulivyo mjini Beirut, hali ni mbaya zaidi. “Hakuna kitu…ni uharibifu mtupu. Ninamaanisha, ni kama eneo la vita. Kama vile bomu la nyuklia limelipuka hapa. Ni vingumu kuamini. Picha haziwezi kuelezea ukweli wa hapa.” 

WFP inasema nyuma ya magofu haya kuna watu wanaotishiwa na njaa. Akiba ya unga wa ngano ambao unategemewa sana nchini Lebanon imesalia kwa angalau kukidhi mahitaji ya wiki sita tu. Matarajio ya WFP ni shehena ya kwanza ya ngano wanayoileta, itafika Lebanon ndani ya siku kumi. Bwana Beasley anasema,  “Asalimia 85 ya chakula chote kinacholetwa Lebanon kinakuja kupitia bandari hii na ni muhimu kuwa tuifanye ifanye kazi tena ili tuweze kuleta vifaa, kila kitu cha muhimu ili kuifanya bandari kufanya kazi tena.” 

Lebanon yapokea msaada kutoka kwa WFP
WFP/Ziad Rizkallah
Lebanon yapokea msaada kutoka kwa WFP

Wakati shehena hiyo ikisubiriwa, tayari WFP inatoa chakula kwa watu walioko hatarini zaidi kote nchini Lebanon ambao kipato chao, kazi na maisha yao yameathiriwa na majanga matatu yaani mlipuko, mdororo wa uchumi na COVID-19.  

Kama hatua ya haraka kufuatia mlipuko mjini Beirut, WFP ilitenga vifurushi vya chakula kwa ajili ya kaya 5,000 zilizokuwa hatarini zaidi na shirika hilo lina mpango wa kuongeza kwa kadri ya mahitaji na wakati huo huo pia wanalisaidia shirika lisilo la kiserikali la Caritas ambalo linawapatia mlo waathirika wa mlipuko na pia wafanyakazi wanaojitolea kusafisha mji. 

Kila kifurushi cha chakula kinatosha kuilisha familia ya watu watano kwa mwezi mmoja na kina vyakula kama vile mchele, maharage, mafuta ya kupikia, sukari, chumvi na vitu vingine muhimu.  

WFP pia inapanga kuwapatia watu 50,000 kote Lebanon, mgao wa chakula kwa kipindi cha miezi sita.