Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatoa msaada kwa watu 40,000 waliotawanywa na machafuko mapya Kivu Kusini

Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.
UNICEF/Madjiangar
Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.

UNICEF yatoa msaada kwa watu 40,000 waliotawanywa na machafuko mapya Kivu Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linatoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa watu 40,000 ambao wamekimbia machafuko ya kikabila katika eneo la milimani la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo watu hao zaidi ya 40,000 wanajumuisha watoto 7,500 wa umri wa chini ya miaka 5 na wanawake wajawazito zaidi ya 1,500, na wamekimbia kutoka katika vijiji vilivyoko Uvira, Fizi na Mwenga wengine tangu mwezi Mei kutokana na mapigano ya kikabila ambayo yameathiri maisha ya maelfu ya watu. 

Katika machafuko hayo UNICEF inakadiria kwamba vituo 10 vya afya viliporwa na kuharibiwa kiasi cha kutoweza kutumika huku vituo vingine 18 vilitelekezwa na wahudumu wa afya kukimbia kwa usalama wao. 

Takriban shule 28 ziliporwa pia au kuharibiwa mwezi Desemba mwaka 2019 na hadi sasa hazijajengwa upya hivyo kuwaacha maelfu ya watoto bila mahali pa kusomea katika jimbo hilo. 

UNICEF na wadau wake kwa sasa wanajikita na kazi na msaada wao katika eneo la Mikenge ambako watu 40,000 wamepata hifadhi katika maeneo ya porini ambako si mbali sana na maeneo walikotoka. 

UNICEF imesaidia kwa kiasi kikubwa kufungua tena hospitali ya Mikenge iliyotelekezwa kwa kuipatia dawa na vifaa tiba vipitavyo tani nne kwa ajili ya kuhudumia watu 20,000 kwa kipindi cha miezi mitatu. 

Pia shirika hilo linatoa chanjo kwa kupitia kliniki za kuhamahama kwa watu 23,000 waliotawanywa na machafuko hayo ambao wamesaka usalama katika mlima Mitumba, kujitahidi kuwaunganisha na familia zao watoto 17 waliotenganishwa na wazazi wao na kutoa vifaa vingine muhimu kwa watoto 300 wa miji ya Mikenge na Bijombo. 

Zaidi ya hapo shirika hilo limesema litatoa tani 4 za mgao wa dharura wa chakula kwa watu 4,000 wasiojiweza wakiwemo kina mama wajawazito, wanawake wanaonyeyesha, wazee na kugawa vitabu na madaftari kwa watoto wasiokwenda shule. 

UNICEF imeonya kwamba hali ni mbaya sana kwa watu waliotawanywa katika milima ya Kivu Kusini  wakihitaji haraka chakula, malazi, huduma za afya na msaada wa elimu, hivyo shirika hilo limetoa wito kwa wadau wa misaada ya kibinadamu kujitoa kusaidia haraka eneo hilo. 

Ombi la fedha la UNICEF kwa ajili ya watoto DRC ni dola milioni 301 lakini hadi kufikia 15 Julai kwama huu ni dola milioni 27,000 tu zilizopatikana na zingine milioni 40 ni za mwaka jana hivyo kuacha pengo kubwa la dola milioni 219 sawa na asilimia 73 ya ombi lote.