Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa wa COVID-19 watafikia milioni 20 wiki hii-WHO 

Mpangilio wa ukaaji na pia ngao za kutenganisha kati ya mtu na mtu vimewekwa ili kuhakikisha umbali kati ya mtu na mtu katika hospitali mjini Bangkok, Thailand
ILO/Alin Sirisaksopit
Mpangilio wa ukaaji na pia ngao za kutenganisha kati ya mtu na mtu vimewekwa ili kuhakikisha umbali kati ya mtu na mtu katika hospitali mjini Bangkok, Thailand

Wagonjwa wa COVID-19 watafikia milioni 20 wiki hii-WHO 

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Dkt Tedros Ghebreyesus ameueleza ulimwengu hii leo kuwa, wiki hii idadi ya wagonjwa wa COVID-19 walioathibitishwa itafikia milioni 20 na vifo 750,000 kote duniani  kwa hivyo viongozi wanatakiwa kuchukua hatua na raia wanatakiwa kuzifuata au kuzikumbatia hatua mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva mapema leo tarehe 10 August, Dkt Tedros amesema, “nyuma ya takwimu hizi kuna maumivu makubwa na mateso. Kila maisha yaliyopotea ni muhimu. Ninafahamu kuwa wengi wenu wanaomboleza na kuwa huu ni wakati mgumu kwa ulimwengu. Lakini ninataka kuwa wazi, kuna matumaini na bila kujali mahali iliko nchi, mkoa, jiji au mji, hakuna kuchelewa kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa.”

Tweet URL


Dkt Tedros ameendelea kwa kusema, “wakati tunashukuru wale ambao wametoa michango, tuko katika  asilimia 10 tu ya njia ya kufadhili mabilioni yanayotakiwa kutekeleza ahadi ushirikiano wa pamoja wa kusongesha maendeleo, uzalishaji, ufikiaji wa vipimo vya COVID-19, matibabu na chanjo.Na hii ni sehemu tu ya uwekezaji wa ulimwengu unaohitajika ili kuhakikisha kila mtu mahali popote anaweza kupata zana. Kwa chanjo pekee, zaidi ya dola za kimarekani bilioni 100 zitahitajika.”

Msaada kwa Lebanon


Kuhusu Beirut, Tedros amesema, “kwa watu wa Beirut, wahudumu wa afya na dharura walioko kazini, fikira zetu ziko pamoja nanyi na tutaendelea kuwaunga mkono.”


Aidha Tedros amesema kuwa  kutoka katika kituo cha mkakati cha WHO kilichoko Dubai, WHO kwa haraka ilituma vifaa vya kupanyia upasuaji na kushughulikia waliopata kiwewe huko Beirut. 


“Tuliachia fedha kutoka mfumo wa dharura na wafanyakazi wetu wako Beirut wakisaidia tathinimi ya madhara ya mlipuko kwa sekta ya afya.  Tunasafirisha vifaa vya kujikinga vya thamani ya dola milioni 1.7 ili kupambana na COVID-19 na misaada ya kibinadamu ambayo iliharibiwa na mlipuko.” Amesema Dkt Tedros.