Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka uchunguzi wa kuaminika na wa wazi kuhusu chanzo cha mlipuko wa Lebanon

Timu ya uokoaji ikiwa kazini  huko  Beirut baada ya mlipuko wa 4 Agosti  2020
© UNOCHA
Timu ya uokoaji ikiwa kazini huko Beirut baada ya mlipuko wa 4 Agosti 2020

UN yataka uchunguzi wa kuaminika na wa wazi kuhusu chanzo cha mlipuko wa Lebanon

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema idadi kubwa ya watu bado hawajapatikana ikiwa ni takriban wiki moja tangu kutokea mlipuko mkubwa nchini Lebanon uliowaacha watu wa taifa hilo na dunia katika majonzi, mshituko mkubwa na hali ya kutoamini kilichojiri. 

Akizungumza kwa njia ya video leo wakati wa kutoa taarifa ya hali ya kibinadamu inayoendelea mjini Beirut  Guterres amesema kwamba “uchunguzi wa kuaminika na wa wazi kuhusu chanzo cha mlipuko huo mkubwa mjini Beiruti ni muhimu. Na matokeo ya mchakato huu lazima yawe ni uwajibikaji unaohitajika na watu wa Lebanon.” 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewakumbusha nchi wanachama kwamba karibu wiki nzima sasa na bado watu wengi hawajulikani waliko na kusisitiza kwamba “Mlipuko huo ulishtua na kushangaza sana”. Kwa mujibu wa duru za Habari takribani watu 158 wamepoteza maisha na wengine 6,000 walijeruhiwa katika janga hilo. 

Mabadiliko 

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kwamba pia ni muhimu kwamba mikakati ya mabadiliko itekelezwe nchini humo ili kukidhi matakwa ya muda mrefu ya watu wa Lebanon. 

Jana Jumapili Umoja wa Mataifa uliandaa mkutano wa kimataifa kwa ajili ya kuisaidia Beirut na watu wa Lebanon kwa kushirikiana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa. 

Guterres amesema mkakati huo umechangisha fedha zinazohitajika kusaidia na kusisitiza ahadi ya kuendelea kushirikiana na wadau wengine kwa ajili ya Lebanon miongoni mwao ni mashirika ya kimataifa ya kibinadamu na umuhimu wa taasisi za kifedha za kimataifa na kikanda katika hili. 

Bandari ya Beirut baada ya mlipuko tarehe 4 Agosti 2020
UNOCHA
Bandari ya Beirut baada ya mlipuko tarehe 4 Agosti 2020

 

Msaada kwa waathirika 

Guterres amesema Umoja wa Mataifa unatathimini na umejizatiti kufuatilia hali haraka kwa msaada zaidi. Kwa mujibu wa vyombo vya Habari mkutano wa kimataifa umechangisha takriban dola milioni 298 ili kutoa msaada wa moja kwa moja kwa waathirika. 

Waandaaji wanatarajia kwamba fedha zilizoahidiwa kwenye mkutano zitasaidia kujikwamua katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, uhakika wa chakula, elimu na makazi. 

Wahisani walioahidi msaada kwa Lebanon ni pamoja na tume ya Muungano wa Ulaya dola milioni 74, Ufaransa dola milioni 59, Qatar dola milioni 50 na Kuwait dola milioni 41. 

Denmark pia imeahidi kusaidia dola milioni 26, Ujerumani dola milioni 20, Cyprus dola milioni 5 na Canada dola milioni 5. Na miongoni mwa nchi ambazo tayari zilishatoa ahadi zao ni Marekani dola milioni 17. 

Mlipuko katika bandari ya Beirut ulisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya makazi
© UNOCHA
Mlipuko katika bandari ya Beirut ulisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya makazi

 

Zahma kubwa 

Matarajio ni kwamba Umoja wa Mataifa utawasilisha ahadi hizo kwa mashirika ya kimataifa na mashirika yasio ya kiserikali NGO’s yanayofanya kazi nchini Lebanon. 

Katika taarifa yake kwenye makao makuu Katibu Mkuu amesisitiza kwamba janga hilo ni kubwa na kwamba limesababisha majonzi makubwa na watu kutoamini kilichotokea. 

Miongoni mwa hatua za misaada ya kibinadamu zilizochukuliwa na Umoja wa Mataifa n Pamoja na kutuma ndege mjini Beirut ikiwa na tani 20 za vifaa tiba. Lengo ni kutoa za haraka 1000 kwa magonjwa mahututi ikiwemo upasuaji kwa watu walioungua vibaya. 

Umoja wa Mataifa pia umeshatoa dola milioni 15 kutoka kwenye fuko la dharura za masuala ya kibinadamu kwenda Lebanon kukidhi mahitaji ya haraka. 

Na awamu ya kwanza ya fedha hizo ilikabidhiwa kwa mamlaka muda mfupi baada ya mlipuko huo Ijumaa iliyopita.