Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa Beirut: Tunapochukua hatua haraka, ndivyo tunaweza kupunguza mateso ya wanadamu-Naibu Katibu Mkuu UN 

Bandari ya Beirut baada ya mlipuko tarehe 4 Agosti 2020
UNOCHA
Bandari ya Beirut baada ya mlipuko tarehe 4 Agosti 2020

Mlipuko wa Beirut: Tunapochukua hatua haraka, ndivyo tunaweza kupunguza mateso ya wanadamu-Naibu Katibu Mkuu UN 

Msaada wa Kibinadamu

Ili kuisaidia Lebanon kuondokana na madhara ya janga na kupona vyema, "tutahitaji ushiriki wa kila mtu," Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed hii leo ameuambia mkutano wa wafadhili uliofanyika kwa njia ya video ili kuisaidia Lebanon kutokana na mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari iliyoko kwenye mji mkuu wan chi hiyo, Beirut na kuwaua watu 150, kujeruhi maelfu na kusababisha uharibifu mkubwa wa sehemu kubwa ya mji. 

“Mlipuko wa Jumanne iliyopita mjini Beirut uliushitua ulimwengu, ukaacha viunga vya mji vikiwa vimesambaratika, kiasi kikubwa cha hifadhi ya nafaka ya Lebanon ilibomolewa, hospitali sita zikaharibiwa , maelfu wamekosa makazi, wengi wao wakiwa ni watoto.” Ameeleza Bi Mohammed kupitia mkutano huo ambao umeitishwa kwa ushirikiano wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Umoja wa Mataifa. 

Aidha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu zake za rambirambi kwa wale ambao wamewapotza wapendwa wao, na kuwatakia maelfu waliojeruhiwa, kupona haraka. 

 

Tweet URL


“Zaidi ya yote, ninatoa ahadi yangu kuwa Umoja wa Mataifa umejitolea kuwasaidia watu wa Lebanon kwa kila njia tunayoweza.” Amesema Amina Mohammed.


Tangu mlipuko ulipotokea, mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi muda wote, kusambaza vifaa tiba, vifaa vya malazi, chakula,pia kuziunganisha familia ambazo zimetenganishwa. 


Pia Bi Mohammed amewashukuru wafadhili ambao wameuwezesha Umoja wa Maraifa kuchukua hatua lakini pia akatahadharisha akisema, “msaada wa kifedha ambao umefika kwa wakati hususani kutoka kwa wadau wa kikanda, tayari unaleta tofauti, lakini huu ni mwanzo,” hii  ikiwa na maana kuwa kwa vyovyote kitahitajika kiasi kikubwa cha fedha.