Funzo kutoka kwa manusura wa Nagasaki lazima yauongoze ulimwengu kuondoa silaha zote za nyuklia-Guterres

9 Agosti 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia maadhimisho ya miaka 75 tangu  bomu la atomiki lilipodondoshwa katika mji wa Nagasaki, Japan, amewasifu hibakusha, yaani waathirika wa shambulio hilo la bomu la nyuklia, ambao wamegeuza shida yao ya miongo kadhaa kuwa onyo juu ya hatari ya silaha za nyuklia na katika mfano wa ushindi wa roho ya mwanadamu.

Bwana Guetteres kupitia ujumbe wake uliowasilishwa na Izumi Nakamitsu ambaye ni Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kudhibiti matumizi ya silaha, amewaeleza manusura akisema, “mfano wenu unapaswa kuupa ulimwengu motisha ya kila siku ya kuondoa silaha zote za nyuklia. Kwa bahati mbaya, robo tatu ya karne baada ya mji huu kuteketezwa kwa bomu la atomiki, tishio la nyuklia linaongezeka tena.”

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia hotuba hiyo ya ameipongeza Nagasaki kuwa ni mfano wa kweli wa uvumilivu, kupona na maridhiano. 

"Raia wa Nagasaki hawaelezewi kwa bomu ya atomiki, lakini wamedhamiria kuhakikisha kuwa janga kama hilo halitawahi kutokea katika mji mwingine au miongoni mwa watu wengine," Guterres  amesema na kuongeza kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kushukuru kwa kujitolea huku kufanikisha ulimwengu bila silaha za nyuklia. 

Katibu Mkuu Guterres ametahadharisha kuwa pamoja na uvumilivu wa watu wa Nagasaki matarajio ya matumizi ya silaha za nyuklia kwa makusudi au kwa bahati mbaya ni ya hatari ya juu.

Amefafanua kuwa kwa kadri silaha za nyuklia zinavyoboreshwa kuwa za kisasa, ngumu, za haraka na hatari zaidi, uhusiano kati ya nchi zenye silaha za nyuklia unaelezewa kuwa wa kutokuaminiana, ukosefu wa uwazi na pia ukosefu wa mazungumzo. 

Bwana Guterres amesema hali  mafanikio katika usitishaji wa silaha za nyuklia yanatishiwa kwa mtandao uliolenga kupunguza hatari za nyuklia na kuzitokomeza, umesambaratika na hivyo akaongeza kuwa, “hali hii ya kutisha inapaswa kubadilishwa.” 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter