Shughuli za uokozi zikiendelea Beiruti ,UN yaonya kuhusu mahitaji lukuki ya kibinadamu 

7 Agosti 2020

Mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yameonya kwamba mahitaji ya haraka ya kibinadamu nchini Lebanon ni makubwa sana kufuatia mlipuko mkubwa uliosambaratisha bandari ya m ji wa Beiruti. 

Duru za hivi karibuni zimesema takribani watu 150 wamepoteza maisha na maelfu kujeruhiwa lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka , wakati huu ambapo waokozi wanaendelea kusaka manusura kwenye vifusi. 

Msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Christian Lindmeier amesema kwamba watu wengi bado hawajulikani waliko na kwamba hospitali zimezidiwa uwezo. 

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya video mjini Geneva Uswisi ameongeza kuwa vituo vitatu vya afya havifanyi kazi na viwili vingine zimeharibika kiasi na kwamba janga hilo limesambaratisha kabisa vitanda 500 vya hospitali. 

Watu bado wamenasa kwenye vifuzi 

Bwana Landmeier ameongeza kuwa “Kipaumbele cha sasa ni huduma ya wagonjwa mahututi na kusaka na kuokoa manusura bila shaka , hilo ni la muhimu sana, bado kuna watu wamenasa katika kifusi na bado kuna watu wako hai chini ya kifusi hicho kulingana na tunayoshuhudia katika vyombo vya Habari na hicho ndio kipaumbele chetu cha kwanza kwa sasa , na bila shaka kuingiza vifaa na misaada , chakula, malazi, pia madawa, vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa mahtuti na pia kwa ajili ya magonjwa yote ambayo hayawezi kutibiwa hospitali kwa sasa”. 

Wakati kukiwa na hofu kuhusu vumbi hatari lililosababishwa na mlipuko huo wa tani 2,750 za gesi ya ammonium nitrate, msemaji huyo wa WHO amewaambia waandishi  wa Habari kwamba wizara ya afya ya Lebanon iliarifu kupungua kwa kiwango cha sumu saa mbili baada ya mlipuko huo. 

UNOCHA
Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka za Lebanon kusaidia uokoaji na masuala mengine baada ya mlipuko mkubwa mjini Beirut uliosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.

 

Kuwasaidia walio hatarini zaidi 

Kipaumbele kikubwa zaidi kinachotia shinikizo ni kupata msaada kwa ajili ya walio hatarini zaidiikiwemo wale wanaohitaji msaada wa huduma za dharura kutoka hospitali ambazo tayari zimezidiwa na wagonjwa wa corona au COVID-19

Kazi hii imekuwa na changamoto zaidi kwani makontena mengi ya kusafirishia mizigo yaliyokuwa yamebeba vifaa vya kujikinga (PPE) vilivyohitajika kwa ajili ya kupambana na janga la COVID-19 vimepotelea kwenye mlipuko. 

“Tunachojua hadi sasa ni kwamba makontena 10 yaliyokuwa na PPE ambayo yalikuwa yamenunuliwa na wizara ya afya yameharibika kabisa. Makontena haya yalikuwa na maelfu kwa maelfu ya barakoa , glavu, magauni ya hospitali  a vifaa vingine muhimu. Tayari tumeshaweka oda kufidia baadhi ya vifaa hivyo na kutoa kipaumbele cha haraka cha kufikisha oda za PPE kwa ajili ya Lebanon kwa sasa” amesema Marixie Mercado msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto aliyeshiriki mkutano huo kwa njia ya video pia. 

Ili kuhakikisha msaada wa haraka unaoendelea WHO imetoa omboi la dola milioni 15. 

Hakuna maji wala umeme. 

Bi Mercado amesenga kuwa takribani nyumba zinazokaliwa na watoto 80,000 zimehabiriwa na mlipuko huo na kwamba nyumba nyingi hivi sasa hazina maji wala umeme. 

Pia amesema wakati huohuo wagonjwa wa COVID-19 wameongezeka huku wagonjwa 255 wakiorodheshwa Alhamisi pekee. 

Hadi kufikia sasa Lebanon imeshuhudia vifo 70 vya COVID-19 na jumla ya wagonjwa 5,672, wakati eneo karibu na ulipotokea mlipuko ni miongoni kwa kitovu cha maambukizi. “Ni vigumu kwa walioambukizwa kujitenga kwa sasa na kuna mahitaji makubwa ya barakoa, lakini kwa watu wengi hivi sasa COVID-19 sio kipaumbele katika fikra zao”. Amesema afisa wa UNICEF wakati akitoa ombi la dola milioni 8.25 kwa ajili ya hatua za dharura. 

Wakimbizi huenda ni miongoni mwa waathirika 

Pia likisaidia kartia hatua za dharura baada ya janga hilo la mlipuko shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linahofia kwamba waathirika wengi wa mlipuko huo wanaweza kujumuisha wakimbizi wanaoishi mjini Beiruti. 

Houssam Yaacoub
Bandari ya Beirut baada ya mlipuko

 

Lebanon inahifadhi jumla ya watu milioni 1.5 waliotawanywa na migogoro wengi wao wakitoka nchi jirani ya Syria. 

“Baadhi ya maeneo yaliyoharibika vibaya na mlipuko huo ni Pamoja na makazi yanayohifadhi wakimbizi. Tumepokea taarifa za awali ambazo bado hatujazithibitisha zikisema kuna vifo vingi miongoni mwa wakimbizi Beiruti, hivi sasa tunashirikiana kwa karibu na timu za uokozi na wahudumu wa misaada ya kibinadamu kusaidia kubaini na kutoa msaada kwa familia za waathirika zinazoomboleza.” amesema Charley Yaxley msemaji wa UNHCR. 

Tathimini ya awali inayoonyesha kuwa maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza nyumba zao au zimeharibiwa vibaya na mlipuko na hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya malazi. 

“UNHCR hivi sasa inatoa akiba yake ya vifaa vya malazi iliyokuwa nchini humo , mahema, milingoti na maelfu ya vifaa vingine vya msaada zikiwemo blanketi na magodoro kwa ajili ya kugawanywa mara moja.” Ameongeza bwana Yaxley. 

Katika hatua za kuongezea nguvu mikakati ya Umoja wa Mataifa ya afya katika kupambana na COVID-19 na janga hili jipya la mlipuko UNHCR imetoa vifaa tiba, mashine za kusaidia kupumua na vitanda kwa ajili ya wagonjwa. 

“Awamu ya pili inaharakishwa hasa katika kuzisaidia hospitali. Msaada huu utasaidia kupunguza shinikizo katika hali ya sasa ambapo hospitali zimezidiwa uwezo na kuruhusu wagonjwa zaidi kutibiwa haraka.” 

Uhakika wa chakula 

Katika suala hilohilo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limetangaza kwamba litaingisha unga wa ngano na nafaka ili kusaidia kuinua hali ya uhakika wa chakula nchini Lebanon wakati nchi hiyo ikijikita katika ujenzi mpya wa bandari ya Beiruti ambako maghara makubwa ya nafaka yamesambaratishwa. 

likitangaza hatua hiyo Ijumaa shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema liko katika majadiliano ya karibu na serikali kuona jinsi ya kuratibu uingizaji huo wa msaada wa dharura. 

Shirika hilo ambalo tayari lina program ya kutoa msaada wa chakula na fedha taslim nchini Lebanon pia linataka kusaidia upande wa kiufundi na utaalam wa mnyororo wa usambazaji misaada. 

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo tayari kuna hofu kwamba mlipuko huo utazidisha hali ambayo ni mbaya ya uhakika wa chakula ambayo imeingiliana na mgogoro wa kifedha na janga la COVID-19 kuwa mbaya zaidi. 

Mtu 1 kati ya 2 ahofia njaa 

Utafiti wa hivi karibuni wa umebaini kwamba chakula imekuwa chanzo kikuu cha hofu nchini Lebanon tangu kutangazwa kwa hatua za kufunga kila kitu kutokana na COVID-19, ambapo mtu 1 kati ya 2 anahofia kutokuwa na chakula cha kutosha. 

Ili kusaidia walio hatarini zaidi shirika hilo linatenga makasha 5,000 ya chakula kwa ajili ya familia zilizoathirika na mlipuko. Kila kasha linatosheleza kulisha familia ya watu watano kwa mwezi mzima likiwa na vyakula vya msingi kama mchele, kunde, makopo ya samaki jotari, chumvi na nyanya za makopo. 

Kutoka hali mbaya hadi mbaya zaidi 

ikielezea hali mbaya inayowaathiri watu wa Lebanon hata kabla ya janga la jumanne ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imeitaka jumuiya ya kimataifa kujipanga na kuisaidia nchi hiyo wakati huu wakikabiliwa na zahma. 

“Wakati eneo kubwa la mji huo halifai kuishi, bandari kuu ya nchi hiyo imesambaratishwa na mfumo wa afya umelemewa , kwa kweli hali ni mbaya sana.” Amesema msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu Rupert Colville. 

Msaada wa fedha 

Na saa chache zilizopita shirika la afya la Umoja wa Mataifa kupitia mkurugenzi wake Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus limetangaza kutoa dola milioni 2.2 kutoka kwenye mfuko wake wa mipango ya masuala ya dharura CFE ili kusaidia mahitaji ya haraka nchini Lebanon. 

“Tunawashukuru sana a wachangiaji wetu wote wa CFE ambao wameturuhusu kuokoa Maisha kupitia hatua za haraka kwa dharura ya kiafya.” Amesema Dkt. Tedross akitangaza kutoa fedha hizo. 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter