Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikakati ya kupambana na COVID-19 na kurejea katika hali nzuri, iwahusishe watu wa asili

 Huko Belize, jamii ya watu wa asilia huchukuliwa kuwa washirika muhimu kwa utunzaji na juhudi za maendeleo endelevu
UNDP/Ya'axche
Huko Belize, jamii ya watu wa asilia huchukuliwa kuwa washirika muhimu kwa utunzaji na juhudi za maendeleo endelevu

Mikakati ya kupambana na COVID-19 na kurejea katika hali nzuri, iwahusishe watu wa asili

Afya

Dunia ikielekea kuadhimisha siku ya watu wa asili keshokutwa Jumapili Agosti 9, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa njia ya video ameeleza kuwa kuna kila haja ya kutambua haki za watu wa asili na kuwajumuisha katika mapambano dhidi ya COVID-19.

Bwana Guterres akianza kwa kueleza namna ambavyo janga la COVID-19 limeziathiri jamii za watu wa asili amesema kihistoria, watu wa asili wamepunguzwa na magonjwa yaliyoletwa katika maeneo yao kutoka kwingine, magonjwa ambayo watu hawa hawakuwa na kinga nayo, “kabla ya janga la sasa, watu wa asili tayari walikuwa wanakabiliwa na ukosefu wa usawa, unyanyapaa na ubaguzi.  Uhaba wa huduma za kutosha za afya, maji safi na kujisafi, vinaongeza hali ya hatari kwao.  Watu wa asili hufanya kazi katika shughuli za jadi na uchumi wa kujikimu au katika sekta zisizo rasmi. Haya yote yameathiriwa vibaya na ugonjwa huu.” 

Guterres akieleza namna jamii za asili zilivyoonesha uimara pamoja na kuathiriwa na COVID-19 amesema jamii asilia zilizo na uhuru wa kusimamia ardhi zao, himaya na rasilimali zao, zimehakikisha uhakika wa chakula na utunzaji kupitia mazao na dawa za jadi.  Akitoa mifano ya baadhi ya jamii hizo, amesema, “watu wa Karen nchini Thailand wamefufua ibada yao ya zamani ya "Kroh Yee" au kufungwa kwa kijiji ili kupambana na janga hili. Mikakati kama hiyo ya kufunga maeneo, imetumika pia katika nchi nyingine za Asia na Amerika ya Kusini.” 

Na kwa msingi huo, Katibu Mkuu Guterres akatoa wito kwa ulimwengu kutambua haki za watu wa asili ambako kunamaanisha kuhakikisha ujumuishwaji wao na ushiriki katika kushughulikia COVID-19 na mikakati ya kurejea katika hali nzuri,  “tangu mwanzo wa janga hili la ulimwengu, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kutetea haki za watu wa asili. Tumekuwa tukisaidia kulinda afya na usalama na kuhakikisha upatikanaji wa ulinzi wa kijamii na fursa za kiuchumi. Mfumo wa Umoja wa Mataifa bado umeazimia kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za watu wa asili na kuongeza msimamo wao wa mnepo.”