Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 Uganda yawa ‘mwiba’ kwa akina mama wanaonyonyesha watoto

Hellen Talemwa, mkazi wa Uganda akiwa na mwanae. Anasema COVID-19 inakwamisha mipango yake ya kumnyonyesha mwanae maziwa ya mama.
UN/ John Kibego
Hellen Talemwa, mkazi wa Uganda akiwa na mwanae. Anasema COVID-19 inakwamisha mipango yake ya kumnyonyesha mwanae maziwa ya mama.

COVID-19 Uganda yawa ‘mwiba’ kwa akina mama wanaonyonyesha watoto

Afya

Maziwa ya mama bado hayajathibitishwa kuwa na uwezo wa kuambukiza virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto," imesema WHO wakati huu ambapo kuna shaka na shuku kuwa yanaweza kusababisha maambukizi.

Wiki ya kimataifa ya unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama ikifikia ukingoni hii leo, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limesema kuwa bado hakuna uthibitisho wowote ya kwamba virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona, au COVID-19, vinaweza kuambukizwa kupitia maziwa ya mama.

Laurence M. Grummer-Strawn, ni Mkuu wa kitengo cha Chakula na Lishe katika mifumo ya afya na anasema, kuwa,  “hatujawahi kuwa na taarifa yoyote, kokote pale duniani kuhusu maambukizi kupitia maziwa ya mama.Tumechunguza maziwa kutoka kwa akina mama wengi, kupitia tafiti mbali mbali. Wakati baadhi ya sampuli za maziwa zinakutwa na chembechembe za virusi na kuonekana kuwa ni chanya, tulifuatilia zaidi na kuchunguza iwapo zinaweza kusababisha maambukizi, ikabainika kuwa hakuna virusi vyovyote vinavyoweza kuambukiza.”

Nchini Uganda ambako bado kuna zuio la kutembea na kuchangamana kutokana na virusi vya Corona, Hellen Talemwa ambaye ananyonyesha mtoto anazungumzia jinsi COVID-19 inampatia changamoto kwenye kumnyonyesha mwanae.

Hellen mkazi wa Hoima anasema kuwa, “changamoto ambazo tumekumbana nazo wakati wa corona sisi wanawake wanaonyonyesha, imekuwa changamoto upatikanaji wa maziwa ya kunyonyesha watoto. Kabla ya mlipuko wa virusi vya corona tulikuwa tunapata milo yote minne inayofaa kwa siku lakini baada ya corona tulianza kupata milo miwili pekee kwani hamna pesa. Hii imeleta changamtoo kubwa katika unyonyeshaji wa mtoto. Changamoto nyyingine imekuwa ni kupeleka watoto hospitalini hasa wanapougua. Unatembea kwa mguu kwenda hospitalini wakati ambapo unaumwa njaa kama mzazi”

Hata hivyo WHO inasema kuwa iwapo mama ana maambukizi ya COVID-19 na hawezi kunyonyesha, basi maziwa yake yakamuliwe na mtoto anyweshwe na kama hilo haliwezekani mtoto anaweza kunyonyeshwa maziwa ya mama mwingine.
 

Ripoti hii imeandaliwa na John Kibego kutoka Uganda na taarifa kutoka WHO