WHO yapeleka misaada ya matibabu Lebanon kuokoa walioathirika na mlipuko

6 Agosti 2020

Ndege iliyosheheni tani 20 za vifaa vya matibabu kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, imetua mjini Beirut, Lebanon ili kusaidia matibabu kwa majeruhi wa mlipuko mkubwa ambao ulitokea juzi tarehe 4 Agosti 2020 katika bandari kuu ya Beirut.

Vifaa hivyo vya matibabu vitasaidia watu waliopatwa na kiwewe na pia kufanya upasuaji kwa watu walio na majeraha na vidonda vinavyotokana na kuungua moto uliosababishwa na mlipuko. 

Shehena hiyo ilibebwa kutoka katika kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa vya WHO mjini Dubai, Falme za Kiarabu mapema jana mchana kwa kutumia ndege iliyotolewa na serikali ya Falme za kiarabu UAE, mdau muhimu wa WHO katika dharura za afya. 

Mwakilishi wa WHO nchini Lebanon Dkt. Iman Shankiti anasema, “mioyo na maombi yetu yako na wale wote walioathirika na tukio hili baya tunapoendelea na mpango wetu wa kuhudumia watu wote nchini Lebanon kwa huduma za kuokoa maisha na huduma muhimu za kiafya. Tunashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za kitaifa za afya, wadau wa afya na hospitali katika kuwatibu waliojeruhiwa na pia kutambua mahitaji ya ziada na kuhakikisha msaada wa haraka.” 

WHO inasema kutokana na mlipuko huo, hospitali 3 mjini Beirut hivi sasa hazifanyi kazi na hospitali nyingine mbili zimeharibiwa kiasi na hivyo kuweka hali mbaya au pengo la uwezo wa hospitali hizo kulaza wagonjwa. Wagonjwa waliojeruhiwa wanahamishwa kwenda katika hospitali nyingine nchini humo kama vile Saida na Tripoli kaskazini, na tayari maeneo mengi ya tiba yamezidiwa. WHO itasambaza vifaa katika hospitali zenye kipaumbele zaidi kote Lebanon, hususani zile zinazopokea na kutibu wagonjwa waliojeruhiwa.  

Dharura hii ya hivi karibuni inakuja katika wakati ambao kumekuwa na machafuko ya hivi karibuni ya kiraia, janga kubwa la kiuchumi, kuzuka kwa COVID-19 na mzigo mzito wa wakimbizi. Kuhakikisha kuwa kuna mwendelezo wa mapambano dhidi ya COVID-19 pamoja na kulenga walio hatarini zaidi kwa misaada ni kipaumbele cha kwanza cha Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon na WHO. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter