Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu kubwa, miaka 75 tangu Hiroshima na Nagasaki bado nchi zinalea nyuklia- Guterres

Mabaki ya jengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki. Majengo yalisalia magofu.
UN /DB
Mabaki ya jengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki. Majengo yalisalia magofu.

Ajabu kubwa, miaka 75 tangu Hiroshima na Nagasaki bado nchi zinalea nyuklia- Guterres

Amani na Usalama

Ikiwa leo ni miaka 75 tangu Marekani iangushe bomu la atomiki kwenye eneo la Hiroshima nchini Japan, Katibu Mkuu wa Umoja waMataifa Antonio Guterres amesema njia pekee ya kuondokana na tishio la nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia. 

Katika ujumbe wake wa siku hii ya leo alioutoa huko Hiroshima nchini Japan kwa njia ya video, Katibu Mkuu amesema amezingatia ukweli kwamba miaka 75 iliiyopita, silaha moja ya nyuklia ilileta vifo na uharibifu katika mji huo. 

“Madhara yake yako hadi leo. Mji na watu wake, hata hivyo wamechagua kutotambuliwa kwa majanga bali kwa mnepo, maridhiano na matumaini. Kama wachechemuzi wa kipekee katika utokomezaji wa silaha za nyuklia, Hibakucha wamebadili janga lao kuwa sauti ya pamoja ya ustawi wa ubinadamu.” 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, mwaka 1945, Umoja wa Mataifa ulitambua umuhimu wa kutokomeza silaha hizo kwa kuwa ni  kipindi hicho hicho janga la mabomu lilikumbwa Hiroshima na Nagasaki. 

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika kudhibiti kuenea kwa silaha  Izumi Nakamitsu (mwenye shada la maua) wakati akihudhuria tukio maalum hii leo  huko Hiroshima kukumbuka shambulio la Hiroshima Japan mnamo Agosti 6, 1945.
Hiroshima City
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika kudhibiti kuenea kwa silaha Izumi Nakamitsu (mwenye shada la maua) wakati akihudhuria tukio maalum hii leo huko Hiroshima kukumbuka shambulio la Hiroshima Japan mnamo Agosti 6, 1945.

Cha ajabu hadi leo lengo hilo bado halijafikiwa, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa, “miaka 75 ni mingi mno kwa kutotambua kuwa umiliki wa silaha za nyuklia unasambaratisha badala ya kuimarisha usalama. Leo hii dunia bila silaha za nyuklia inaonekana kutuponyoka mikononi mwetu. Mtandao wa udhibiti wa silaha, uwazi na kanuni za kujengeana imani vilivyoanzishwa wakati wa vita baridi na baada ya hapo vinafifia. Mgawanyiko , ukosefu wa imani na mazungumzo vinatishia kurejesha dunia yetu katika ushindani wa nyuklia usio na maana yoyote.” 

Katibu Mkuu amesema kuwa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zinazidi kuimarisha makombora yao na hatari ya nyuklia kutumiwa kwa makusudi au kwa bahati mbayá ni kubwa kwa mienendo hiyo kuendelea. 

“Natoa wito kwa serikali kurejea katika dira ya pamoja na mwelekeo wa kutokomeza kabisa silaha za nyuklia. Wakati nchi zote zinaweza kuwa na jukumu chanya, nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zina wajibu wa kipekee. Kila mara zimejizatiti kutokomeza silaha za nyuklia. Sasa ni wakati wa mazungumzo, kuweka mikakati ya kujengeana imani, kupunguza ukubwa wa silaha zao za nyuklia na zaidi ya yote kujizuia kuzitumia.” 

Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo, picha hii ilipigwa  umbali wa kilometa 3 kutoka kitovu cha bomu hilo.
UN /Nagasaki International
Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo, picha hii ilipigwa umbali wa kilometa 3 kutoka kitovu cha bomu hilo.

 

Ametaka pia kulinda na kuimarisha mifumo ya kimataifa ya kuendeleza matumizi ya nyuklia akisema kuwa mwakani serikali zitakuwa na fursa hiyo wakati wa mkutano wa mapitio ya mkataba wa kuzuia kuenea kwa nyuklia au NPT. 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa kila mtu ana jukumu katika kutokomeza silaha za nyuklia akisema vijana na mashirika ya kiraia wamethibitisha nguvu yao mara kwa mara katika kuunga mkono kutokomeza silaha za nyuklia. 

“Tunapaswa kusikiliza mawazo yao na kuwapatia fursa ili sauti zao zisikike. Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi na wale wote wanaosaka kufanikisha lengo letu moja la kuwa na dunia bila silaha za nyuklia.” 

Mwaka 1945 Marekani iliangusha mabomu ya nyuklia katika miji ya Hiroshima na Nagasaki. Hiroshima ilikuwa tarehe 6 Agosti 1945 ilhali Nagasaki ilikuwa tarehe 8 Agosti 1945. 

Muhammad- Bande apaza sauti

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Matiafa, Tijani Muhammad-Bande yeye amesema kuwa ni dhahiri shairi kuwa hakuna mshindi katika vita vya nyuklia.

Tweet URL

Akihutubia Baraza Kuu kwa njia ya video katika tukio la kumbukizi ya siku hiyo hii leo, Profesa Muhammad-Bande ameambia nchi wanachama kuwa, “lazima tuahidi tena katika kuondokana na silaha yza nyuklia kwa kuwa katu hakutawepo na uhalalisho wowote wa madhara yatokanayo na silaha za nyuklia. Lazima kila mtu ajizatiti kufanya hivyo.”

Akiuita mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia kuwa ni mkataba wa kihistoria, kwenye kuondokana na nyuklia, Rais huyo wa Baraza Kuu ametoa wito kwa nchi wanachama kutia saini na kuridhia mkataba huo.

Kwa waliopoteza maisha katika shambulio la Hiroshima na Nagasaki, Rais huyo amesema, “katika kuwakumbuka, hebu na tufanye kazi pamoja kuwa na mustakabali tuutakao, mustakabali usio na tishio la silaha za nyuklia.”

CTBTO nayo yasema Nagasaki na Hiroshima bado ni mzimu

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Shirika la Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya silaha za Nyuklia, CTBTO, Lassina Zerbo, amesema milipuko ya kutisha ya Hiroshima tarehe 6 Agosti na Nagasaki tarehe 8 Agosti 1945 bado imesalia katika fikra za binadamu na kuibua swali tete: Je tunaweza kuondokana na fikra zilizosababisha kutokea kwa milipuko hiyo ya mabomu?

Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani  ya UN, jijini New York, Marekan
UN/Jihye Shin
Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani ya UN, jijini New York, Marekani

Akiwaita hibakusha, kuwa ni kichocheo thabiti cha utu, amesisitiza kuwa machungu yao na simulizi zao vimefanya hatari ya nyuklia kuonekana dhahiri na kwa uwazi.

Kwa mujibu wa Bwana Zerbo, hibakusha ambao ni manusura wa mashambulio ya Hiroshima na Nagasaki, wamefundisha uvumilivu, azma na azimio kuwa ni vitu muhimu katika kufanikisha malengo ya muda mrefu ya kuondokana na nyuklia.

“Lazima tumalize kile tulichoanza kwa sababu kile kilichotokea Japan katu kisitokee tena,” amesema Zerbo akiongeza kuwa lazima tuwasikilize ili tuweze kuchukua hatua.