WFP wajitosa kuisaidia Lebanon kwani bila bandari ya Beirut, hali itakuwa mbaya zaidi

6 Agosti 2020

Ikiwa leo ni siku ya pili tangu kutokea kwa mlipuko mkubwa katika bandari mjini Beirut, Lebanon, shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema linafanya tathimini ya haraka ili kujiweka tayari kutoa msaada wa dharura kwa maelfu ya watu ambao wamejikuta katika hali ya kukosa makazi, wamejeruhiwa na pia wamewapoteza wapendwa wao.

Bandari ya Beirut na sehemu kubwa ya mji huo imeachwa na magofu na vilio vya kila namna. WFP inasema Lebanon hata kabla ya tukio hilo la kusikitisha, ilikuwa tayari katika hali mbaya ya uchumi kuwahi kutokea katika historia yake na hali hiyo ilikuwa inafanywa kuwa mbaya zaidi na janga la COVID-19

Uharibifu mkubwa uliosababishwa na mlipuko huo katika bandari hii kubwa zaidi nchini Lebanon, kutapaisha zaidi bei ya vyakula kufikia kiwango ambacho si wengi wataweza kukimudu kwani nchi hiyo inaagiza chakula chake kutoka nje kwa asilimia 85 na kwa kiasi kikubwa kinapokelewa katika bandari ya Beirut. 

Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka za Lebanon kusaidia uokoaji na masuala mengine baada ya mlipuko mkubwa mjini Beirut uliosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.
UNOCHA
Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka za Lebanon kusaidia uokoaji na masuala mengine baada ya mlipuko mkubwa mjini Beirut uliosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa.

Kapteni Joinal Abedin kutoka kikosi kazi cha majini, MTF  cha ujumbe wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL ambao moja ya meli yao imeharibiwa na baadhi ya maafisa wake kujeruhiwa, anaeleza alivyoshuhudia tukio hilo, anasema,“ilikuwa siku ya kawaida, kila mtu alikuwa anafanya kazi yake na watu walikuwa wanazunguka hap ana pale wakitekeleza majukumu yao na ghafla tukaona kuna moto mdogo. Kwa hivyo moto mdogo haimaanishi kutakuwa na uharibifu. Baada ya dakika mbili moto ukaja karibu na tulikuwa bado tunaona ni kawaida kisha ghafula kukawa na mlipuko mkubwa ambao ulitokea ndani ya sekunde chache. Sijui namna mlipuko wa Hiroshima ulivyokuwa, lakini ulikuwa karibu sawa na huo.” 

Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za Lebanon ili kusaidia kukabiliana na matokeo ya mlipuko huo mkubwa ambao umetokea huku raia milioni moja wa Lebanon wakiishi chini ya mstari wa umasikini yaani chini ya dola moja kwa siku. 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter