Theluthi mbili ya wakimbizi milioni mbili wa Sudan Kusini ni watoto-UNHCR

5 Agosti 2020

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR zinaonesha kuwa theluthi mbili ya raia milioni mbili wa Sudan Kusini wanaoishi uhamishoni, ni watoto.

UNHCR inaonesha namna migogoro inavyosababisha matatizo kwa familia na watoto kwani watoto wanalazimika kuvuka mipaka wakiwa hawana usimamizi, na hivyo kukumbana na matatizo makubwa zaidi. Nchini Ethiopia kwa mfano, watoto wakimbizi 42,000 walivuka kutoka Sudan Kusini bila usimamizi wowote au wametenganishwa na familia zao. Katika kambi ya wakimbizi ya Jewi nchini Ethiopia, wasichana wawili ndugu raia wa Sudan Kusini wanajaribu kujenga maisha mapya ugenini baada ya kuikimbia nchi yao, huyu ni Nyamach anasema, 

“Tulifuata tu makundi ya watu. Ilikuwa vigumu sana. Tulikimbia bila chochote. Tulipofika, tulipewa usaidizi na nguo kadhaa.” 

Nyamach Lul ameyajua machungu katika miaka yake 16 duniani pengine kuliko hali wanayokutana nayo watu wengine wengi katika maisha yao yote. Barubaru huyu kwanza alifiwa na baba yake katika shambulizi lililofanywa na kundi lililojihami kwa silaha, na kisha akampoteza mama yake kutokana na kuugua. Mtu pekee ambaye amesaliwa naye kwa muda wote ni mdogo wake wa kike mwenye umri wa miaka 13, Nyakoang.  

Kwa miaka mitatu iliyopita, wawili hawa wamejitengenezea nyumba yao katika kambi ya Jewi, moja ya kambi nane zinazowatunza zaidi ya wakimbizi 300,000 raia wa Sudan Kusini katika mkoa wa Gambella magharibi nchini Ethiopia. Nyamach anaanda chakula kwa ajili yake na mdogo wake,  

“Ninajihisi kuwajibika. Tunapokuwa hatuna chakula cha kutosha, ninamwacha mdogo wangu ale kwanza. Ninapenda kumwona akifurahi.” 

Mdogo wake anasema, “ananijali vizuri. Ninampenda dada yangu.”  

Ndugu hawa waliikimbia Sudan Kusini mwaka 2016 wakiwafuata maelfu ya watu wengine ambao walikuwa wanayakimbia mauaji, ubakaji na vijiji kuchomwa moto na pande zinazopiagana. Nyamach anasema anapocheza na watoto wenzake anafurahi kwani inamsahaulisha machungu kiasi na ana matumaini kuwa siku moja atapata kazi nzuri aendelee kumtunza mdogo wake.  

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud