Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapeleka timu kutathmini tukio la shambulio la alfajiri kambini Cameroon ambako watu 18 wameuawa

Wakimbizi kutoka Nigeria wakiwasili katika kijiji cha Goura nchini Cameroon mwezi Januari 2019
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wakimbizi kutoka Nigeria wakiwasili katika kijiji cha Goura nchini Cameroon mwezi Januari 2019

UNHCR yapeleka timu kutathmini tukio la shambulio la alfajiri kambini Cameroon ambako watu 18 wameuawa

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limelaani vikali mauaji ya watu wapatao 18 katika kambi ya muda ya kuhifadhi wakimbizi wa ndani nchini Cameroon. 

Mauaji hayo yanatokana na shambulio la kikatili katika kambi hiyo iliyoko karibu na kijiji cha Nguetchewe kwenye jimbo la Kaskazini ya Mbali nchini Cameroon, shambulio lillilofanywa alfajiri ya tarehe 2 mwezi huu wa Agosti wakati wakimbizi wakiwa wamelala.

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video hii leo mjini Geneva, Uswisi, amesema kuwa wakimbizi wengine 11 walijeruhiwa baada ya kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kurushwa kwa mkono kuangukia kwenye kambi hiyo inayohifadhi wakimbizi 800.

Majeruhi walisafirishwa hadi hospitali ya wilaya ya Makolo, umbali wa saa moja kwa gari kutoka Nguetchewe, huku watu wapatao 1,500 wakiweko wenyeji waliokuwa na hofu wakilazimika kukimbilia mji jirain wa Mazogo ili kunusuru maisha yao.

Bwana Baloch amesema kuwa, “UNHCR inapeleka timu ya dharura kutathmini hali ilivyo na kubaini mahitaji ya ulinzi na kiafya ya wale walioathiriwa. Jamii enyeji katika eneo hili maskini mara nyingi ndio wanaokuwa waokoaji wa kwanza wa wale wanaokimbia ghasia kwenye eneo hilo la ziwa Chad na kaskazini-mashariki mwa Nigeria.”

Ameongeza kuwa kutokana na hali hii ya awali ya ukosefu wa usalama, UNHCR inatarajia huduma za ulinzi wa jamii, malazi, maji na huduma za kujisafi zitapaswa kuimarishwa wakati huu ambapo Cameroon inakabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Bwana Baloch amesema wanatoa wito kwa pande zote kuheshimu kanuni za kambi za wakimbizi wa ndani na wahudumu wa kibinadamu kambini na kuchukua hatua za haraka kutimiza mahitaji ya watu waliokimbia ghasia.

Shambulio la Jumapili linafuatia ongezeko la matukio ya ghasia kwenye eneo hilo la Kaskazini ya Mbali la Cameroon mwezi uliopita wa Julai, likiwemo tukio la uporaji na utekaji nyara uliofanywa na kikundi cha Boko Haram na vikundi vingine vilivyojihami kwenye eneo hilo.

Jimbo la Kaskazini ya Mbali la Cameroon liko kati ya majimbo ya Nigeria ya Borno na Adamawa na Ziwa Chad na lina wakimbizi wa ndani 31,886 na wakimbizi 115,000 kutoka Nigeria.