Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Wayazid kwa kuwa na mnepo baada ya mauaji ya kimbari:UNAMI

Myazidi kutoka Sinjar  nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani  ya Mamilyan  huko Akre, nchini Iraq
Giles Clarke/ Getty Images Reportage
Myazidi kutoka Sinjar nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mamilyan huko Akre, nchini Iraq

Heko Wayazid kwa kuwa na mnepo baada ya mauaji ya kimbari:UNAMI

Amani na Usalama

Leo ni miaka sita ya kumbukumbu ya kampeni ya mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa na kundi la kigaidi la Da’esh au ISIL dhidi ya jamii ya kabila la wachache la Wayazid nchini Iraq.

Akikumbuka mauaji hayo mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq ambaye pia ni mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNAMI, Jeanine Hennis-Plasschaert, amewapongeza jamii ya Wayazid kwa mnepo walionao kwa kulinda ardhi na utamaduni wao na dhamira ya kusaka haki zao kwa njia yoyote ile. 

Pia ameitaka malaka Baghdad na Erbil kufikia muafaka bila kuchelewa wa kuwazipa nyenzo jamii za Wayazid na kuziwekea mazingira mazuri ya kujenga upya Maisha yao. 

Mwaka 2014 kundi la Da’esh (ISIL) lilivamia mji wa Sinjar na kuua na kusambaratisha katika kampeni maalum wakiwalenga jamii ya Wayazid. Maelfu kwa maelfu ya watu walikimbilia milimani na wengi waliuawa. 

Ameongeza kuwa “wanawake na Watoto wakitekwa na kufanywa watumwa huku wakipitia ukatili mkubwa wa kingono. Na wengine wengi bado hawajulikani waliko hadi sasa na manusura wanaendelea kubeba makovu makubwa ya unyama walioupitia.” 

Ripoti ya UNAMI imesema wanawake hasa walikuwa wahanga wakubwa wakinyanyapaliwa na kukataliwa na mpaka leo wanaendelea kughubikwa na jinamizi la ukatili huo na kukabiliana na changamoto za kisiasa, kiusalama na kiuchumi zilizosababishwa na mauaji ya kimbari, lakini hata hivyo jamii hiyo ya Wayazid imejizatito kujenga mustakabali bora. 

Bi. Hennis-Plasschaert amesema “Ninatiwa moyo na dhamira ya Wayazid wengi ya kusaka uhuru na haki kwa ajili ya jamii yao. Hata hivyo changamoto yao haijaisha, Wasinjar wanaendelea kuteseka kuanzia katika masuala ya usalama, kutokuwepo na huduma za kutosha na kukosekana kwa muungano wa uongozi.” Amehoji kwamba “Kwa nini tuendelee kulipa gharama kubwa ? tukifahamu fika kwamba suluhu endelevu inawezekana?” 

Amerejelea kutoa wito kwa serikali za Baghdad na Erbil kutatua haraka suala hili na kufikia muafaka bila kuchelewa. “Serikali imara na mifumo ya usalama ni msingi muhimu kwa jamii kujijenga upya na kushamiri. Tuna deni hilo kwa manusura. Tuna deni hilo kwa utu wetu wa pamoja.”