Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu pekee haitoshi kumaliza janga la njaa:IFAD

Umoja wa Mataifa na harakati za kusaidia kuhakikisha uhakika wa chakula.
IFAD/GMB Akash
Umoja wa Mataifa na harakati za kusaidia kuhakikisha uhakika wa chakula.

Misaada ya kibinadamu pekee haitoshi kumaliza janga la njaa:IFAD

Msaada wa Kibinadamu

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD umesema misaada ya kibinadamu pekee haitoshi kushughulikia janga kubwa la njaa linaloizogoma dunia hivi sasa kunahitajika hatua za kuijengea jamii mnepo kukabili janga hilo

Makamu wa rais mpya wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD Dominik Ziller katika siku yake ya kwanza ofisini hii leo mjini Roma Italia amesema misaada ya kibinadamu haitoshi kushughulikia suala la ongezeko la njaa. 

Bwana Ziller amesema, “tunafahamu kuwa COVID-19 itaongeza sana njaa na umaskini hususani katika maeneo ya vijijini. Hii ni kwasababu watu wengi wa vijijini wanaishi kwa kutegemea mnyororo wa kilimo kwa ajili ya kipato chao na chakula, na mnyororo huu wa usambazaji umevurugika.Haitoshi kushughulikia suala hili kwa misaada ya kibinadamu pekee. Tunapaswa kujenga minyororo ya usambazaji ambayo inaweza kuhimiri majanga vinginevyo watu wataendelea kwenda vitandani na njaa.” 

Aidha Mkuu huyo wa IFAD amekumbusha  kuwa miaka mitano iliyopita jumuiya ya kimataifa iliahidi wakati ilipoidhinisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, kutokomeza umasikini na njaa lakini sasa mipango iko nje ya njia katika kufikia lengo la kutokomeza njaa na ni miaka 10 tu imesalia kutimiza ahadi.Na kwa hivyo hatuwezi kuweka mikono yetu chini na kukata tamaa. Tunatakiwa kwenda hatua nyingi zaidi.  Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi uliopita wa Julai kuhusu hali ya uhakika wa chakula na lishe duniani, njaa imeongezeka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na matokeo ya janga la COVID-19 yanategemewa kuwaacha watu milioni 83 zaidi ya wale milioni 132 wenye njaa kufikia mwisho wa mwaka huu.  

Kiongozi huyo ameahidi kuutumia uzoefu wake wa kufanya kazi katika serikali ya Ujerumani kama Mkurugenzi Mkuu wa ushirikiano wa maendeleo kimataifa kupitia wizara ya ushirika wa uchumi na maendeleo ya Ujerumani BMZ, ili kuisaidia IFAD kufikia lengo la kutokomeza njaa.