UNICEF na IKEA wasaidia kuboresha lishe ya mama na mtoto India

3 Agosti 2020

Wiki ya unyonyeshaji duniani ikiendelea shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema sikua 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama yake ni muhimu sana katika ukuaji wa ubongo hali ambayo itaamua mustakabali wa mtoto, jinsi gani anafikiri, kujifunza na tabia yake na lishe muafaka ikiwemo maziwa ya mama ni ufunguo wa kila kitu. 

Katika wilaya ya Udaipur jimboni Rajasthan nchini India Pyari Nayakheda akijiandaa kumuweka mwanaye mchanga nje kwenye bembea ili aendelee na shughuli zingine akimsubiri mkunga kuja kumtembelea kujua hali yake na mtoto. 

UNICEF kwa msaada wa wakfu wa IKEA umewawezesha wahudumu wa afya katika kituo cha Anganwadi kwa mafunzo ya lishe bora lengo likiwa ni kuwasaidia wazazi na wahudumu wa nyumbani kutoa huduma inayostahili kwa watoto tangu mama akiwa mjamzito, anapojifungua na hata baada ya kujifungua. 

Wasichana vigori katika wilaya ya Udaipur India
UNFPA India/Arvind Jodna
Wasichana vigori katika wilaya ya Udaipur India

Vilma Kapoor ni muuguzi na mkunga katika kituo cha afya cha Anganwadi ambaye amekuwa akipita nyumba kwa nyumba kuelimisha kina mama wajawazito na wenye watoto kuhusu lishe bora anasema “Asilimia 30 hadi 40 ya maendeleo ya mtoto yanafanyika akiwa tumboni, na mtoto anaanza kupokea huduma tangu akiwa tumboni mwa mama yake.” 

Shaheen na Altaf wanatarajia kupata mtoto hivi karibuni na wamekuwa wakihuhuria kliniki kwenye kituo cha Anganwadi kupata ushauri kuhusu lishe na wanasema vyakula mchanganyiko kama maziwa, mboga za majani, na mayai ni muhimu kwa Shaheen na mtoto alyembeba tumboni na wanaimani kwamba hata atakapojifungua mtoto atakuwa na afya njema. 

Mfumo wa chanjo na ufuatiliaji umesaidia India kupunguza idadi ya vifo vya watoto ambao hawajatimiza umri wa miaka 5
UNDP India
Mfumo wa chanjo na ufuatiliaji umesaidia India kupunguza idadi ya vifo vya watoto ambao hawajatimiza umri wa miaka 5

Pyari Nayakheda alipatiwa mafunzo ya lishe bora akiwa mjamzito na sasa amejifungua salama na mwanaye ana afya njema “Nambeba mwanangu na ninamsemesha. Nilianza kuhudhuria kituo cha Anganwadi nikiwa na ujauzito wa miezi mitatu. Mkunga amekuwa akinipa ushauri tangu wakati huo, alikuwepo nilipojifungua na bado yuko nami. Kwa miezi sita ya mwanzo nilishauriwa kumpa mwanangu maziwa ya mama tu na baada ya hapo nikamuanzishia vyakula vingine. Hivyo mwanangu hupata virutubisho pia kutokana na kile ninachokula. "

Kituo cha Anganwadi mbali ya kutoa huduma za afya na lishe pia kinatoa huduma na malezi ya watoto wadogo wa wilaya ya Udaipur ambapo wanafundishwa kusoma na kuhesabu kwa tumia mbinu mbalimbali lakini pia kucheza. 

Mradi huo umeshatoa mafunzo kwa wahudumu zaidi ya 8,000 na elimu na huduma ya elimu ya lishe wanayoitoa imeleta tija kubwa wa kina mama na watoto wao na sasa jimbo la Rajasthan limeamua kuiga mfumo huo na kuusambaza katika wilaya zote. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter