Skip to main content

SOFEPADI na harakati za kusaidia wahanga wa ukatili wa kingono DRC

Marie-Noelle mwenye miaka 22, mjane mwenye watoto watatu na manusura wa ukatili wa kingono DRC, ni mmoja wa wanajumuiya wa umoja wa kina mama wa Mokolo kikundi kinachowasaidia wanawake na kuwawezesha.
UN Women/Ryan Brown
Marie-Noelle mwenye miaka 22, mjane mwenye watoto watatu na manusura wa ukatili wa kingono DRC, ni mmoja wa wanajumuiya wa umoja wa kina mama wa Mokolo kikundi kinachowasaidia wanawake na kuwawezesha.

SOFEPADI na harakati za kusaidia wahanga wa ukatili wa kingono DRC

Wanawake

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC matukio ya ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji yanaendelea kutekelezwa kimfumo na vikundi vinavyopigana kwenye taifa hilo lililoshuhudia mapigano mara kwa mara.

Matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kupitia ripoti za Umoja wa Mataifa yakitajwa kuwa ni uhalifu siyo tu kwa mujibu wa sheria za DRC bali pia sheria za kimataifa. 

Hata hivyo baadhi ya manusura wa vitendo hivyo wamekuwa wakihaha kupata haki ambapo shirika la kiraia la SOFEPAD linalohusika na usaidizi kwa wanawake na watoto waliobakwa, limechukua hatua kusaidia manusura hao. 

Élisabeth Furaha, ni daktari kwenye kliniki shirika hili na anasema kuwa, “sisi ndio tunaokutana na waathiriwa wa ukatili wa kingono kwa mara ya kwanza baada ya tukio. Kwa mwezi Januari pekee, tumepokea waathirika 46 wa ukatili wa kingono tumewapatia dawa za virusi vya UKIMWI, vidonge vya kuzuia mimba zisizotakiwa. Wanapata pia kipimo cha kujua iwapo wamepata ujauzito au la na pia vipimo vya UKIMWI.” 

Kwa Noëlla Alifwa, ambaye ni mmoja wa waasisi wa SOFEPADI hali wanayoiona inakuwa si nzuri kwa kuwa, “watu wanaofika hapa wamebakwa, wameteswa, wamejeruhiwa. Na kile ambacho ni kigumu kwetu ni kwamba hivi karibuni tumeona watoto ambao wameuawa.” 

Manusura wanawake na watoto, kutokana na machungu waliyopitia inakuwa vigumu sana kusimulia yaliyowakumba na hata kutaja jina, hivyo SOFEPAD imeajiri mwanasaikolojia Espérance Karungi. 

Bi. Karungi anasema kuwa, Tupo hapa kusaidia wagonjwa, tunapowapokea, kwanza tunasikiliza shida zao. Tunasaka majawabu, tunatafuta mzizi wa tatizo, tunafanya yote haya kwa pamoja na mgonjwa ili wao wenyewe waweze kuamua kile cha kufanya, sisi hatupo hapa kuwaeleza cha kufanya.” 

Miongoni mwa wateja wa leo ni mwanamke mmoja anayefanya kazi mashambani ambaye yeye na binti yake walibakwa, na sasa kwa pamoja wanamlea mtoto aliyezaliwa kutokana na kitendo hicho. 

Wateja wao wanapatiwa pia msaada wa matibabu na kisheria ambapo Gloria Malolo anayefanya kazi na ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na DRC ya haki za binadamu yenye mamlaka ya kusaka haki na fidia kwa waathirika wa ubakaji na wanafanya kazi kwa ushirikiano na kliniki ya SOFEPADI. 

 “Tunaweka kumbukumbu ya kesi hizi ili tuweze kuziwasilisha kwenye mfumo wa sheria, hasa ule wa kijeshi, kwa kuwa wao wana uwezo wa kuamua kuhusu makosa yaliyofanywa na vikundi vilivyojihami au jeshi la serikali. Baada ya hapo wanawajibika, kama mamlaka, kuweka kumbukumbu na kuchunguza ukiukwaji huu wa haki za binadamu, ametamatisha Gloria.