Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumikishwaji wa kingono, ukahaba – Kunusuru manusura wa usafirishaji haramu binadamu Malawi

Soko la Lunzu kusini mwa Malawi
WFP/Greg Barrow
Soko la Lunzu kusini mwa Malawi

Utumikishwaji wa kingono, ukahaba – Kunusuru manusura wa usafirishaji haramu binadamu Malawi

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa unasaidia serikali ya Malawi kukabiliana na tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu wakati huu ambapo ripoti zinaonesha kuwa taifa hilo la kusini mwa Afrika limegubikwa na utumikishaji wa wavulana mashambani, utumikishaji wa wasichana kwenye vilabu vya  usiku ambako hulazimishwa kufanya ngono.

Taarifa zinataja wanaume 6 kutoka Nepal ambao waliaminishwa kuwa wanasafirishwa kwenda Marekani kwa ajili ya kazi, lakini badala yake wakajikuta kwenye safari ndefu iliyowapitisha mataifa mbali mbali hadi kuishia Malawi ambako walifungiwa kwenye nyumba moja na kupokonywa hati zao za kusafiria. 

Mume na mke waliahidiwa kazi nzuri katika shamba kubwa la tumbaku katika nchi jirani Zimbabwe ambako pindi baada ya kuwasili walikumbana na mateso na kunyimwa chakula na hawakupatiwa malipo yoyote mwishoni mwa mkataba wao. Kazi waliyoifanya tofauti na waliyoahidiwa ambako walilazimishwa kutumbukia kwenye ukahaba. 

Watu hao wote ni manusura wa usafirishaji haramu ambapo Malawi inatajwa kuwa ni kituo cha mpito cha watu wanaosafirishwa kwenye mataifa mengi ya Afrika yakiwemo Afrika Kusini, Tanzania, Msumbiji na maeneo mengine ya Ulaya. “Serikali ya Malawi inakubali kuwa hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kukabili uhalifu huu na kuziba mapengo kwenye mkakati unaotumika sasa,”  amesema Maxwell Matewere, Afisa wa kitaifa wa mradi unaotekelezwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC nchini Malawi. 

Kufuatia ombi la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Malawi la kutaka msaada wa kutekeleza Sheria ya Kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu nchini humo, iliyoandaliwa kwa msaada na UNODC, Bwana Matewere hivi karibuni alitumia wiki tatu kusaidia kujenga uwezo wa maafisa wa polisi. “Mafunzo yalifanyika Blantyre, Phalombe na Mchinji. Haya ni maeneo yenye idadi kubwa ya matukio ya watu kusafirishwa kiharamau,” amesema Bwana Matewere. 

Eneo la kati la manunuzi ya bidhaa kwenye mji mkuu wa Nepal, Kathmandu
World Bank/Peter Kapuscinski
Eneo la kati la manunuzi ya bidhaa kwenye mji mkuu wa Nepal, Kathmandu

Wakati wa mafunzo hayo, mtaalamu huyo kutoka UNODC alipitia upya matukio na kuona iwapo maafisa wa polisi walifuata kanuni sahihi. “Tulibaini kuwa katika matukio mengi, hilo halikufanyika lakini ilikuwa inatia moyo kuona ari ya washiriki,”  amesema Bwana Matewere, akiongeza kuwa “wote wameazimia kuboresha maeneo ambako ni dhaifu ambayo tulibaini wakati wa mafunzo yetu.” 

Washiriki walikuwa ni maafisa wanaohusika na udhibiti wa usafirishaji haramu wa binadamu, uchunguzaji wa kesi na kusaidia manusura bila kusahau waendesha mashtaka. “Nimejifunza kuhusu viwango vinavyotakiwa kuzingatiwa na kanuni ili kusaidia msaada kwa manusura,” ameeleza Stephano Joseph, ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii mjini Blantyre na kuongeza kuwa atafuata kanuni hizo katika majukumu yake. 

Caleb Ng’ombo, Mratibu wa kamati ya pamoja ya mashirika dhidi ya usafirishaji haramu binadamu mjini Blantyre amesema kuwa wamejifunza mambo mengi wakati wa mafunzo hayo ikiwemo umuhimu wa kuweka mbele mahitaji na haki za manusura.

Hivi sasa Bwana Matewere anasema kuwa tayari anapokea ripoti za washiriki wa mafunzo hayo kutumia kile walichojifunza kwenye kazi zao za kila siku. “Kulingana na mwongozo niliotoa, watu 52 wamenusurika na vitendo vya usafirishaji haramu nchini Malawi na watuhumiwa watano wamekamatwa. Kuna matukio matano tofauti ambapo matatu yalibainika wakati wa mafunzo na kwa usaidizi wangu wa kiufundi,” amesema Bwana Matewere.